RAUNDI YA TATU IKIENDELEA, KWA MKAPA MOTO KUWAKA TENA LEO

Raundi ya tatu ya Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa michezo miwili, Mtibwa Sugar watawakabili Ihefu SC kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro saa 10:00 Alasiri huku saa 1:00 usiku Simba SC wakicheza na KMC FC kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Wakizungumza na waandishi wa habari makocha wa Simba na KMC wamesema hali ya vikosi vyao ipo vizuri kuelekea mchezo huo.

“hatuna majeruhi yoyote ndani ya kikosi chetu wachezaji wote wapo tayari kwa mchezo isipokua Josh Onyango ambaye hakufanya mazoezi na timu “. alisema Selemani Matola Kaimu Kocha Mkuu wa Simba.

Naye Kocha Msaidizi wa KMC Ahmad Alli alisema ” Tunawaheshimu Simba kwasababu ni timu bora, licha ya kutokua na rekodi nzuri mbele yao ila tunakwenda kutafuta alama dhidi yao ‘.

KMC hawajawahi kupata alama yoyote mbele ya Simba katika michezo yote nane ya Ligi Kuu ya NBC tangu walipopanda msimu wa 2018/2019.

Hapo jana mchezo wa kwanza wa ‘Derby’ Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2022/2023 kati ya Yanga SC na Azam FC ulimalizika kwa sare ya mabao mawili kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, mabao yote mawili ya Yanga yalifungwa na Feisal Salum dakika ya 56 na 76 huku yale ya Azam yakifungwa na Daniel Amoah na Malickou Ndoye katika dakika ya 24 na 65.

Yanga wanaendeleza rekodi yao ya kucheza michezo mingi ya Ligi Kuu ya NBC bila kufungwa wakifikisha michezo 40.

Mapema saa 10:00 alasiri kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Geita Gold walikua wenyeji wa Kagera Sugar na mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao moja, bao la Geita Gold lilifungwa na Seleman Ibrahim dakika ya 74 wakati lile la Kagera Sugar likifungwa na Abeid Athuman dakika ya 44.

 

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *