Wakazi wa jiji la Mbeya na viunga vyake leo Septemba 9, 2022 wanakwenda kushuhudia ‘derby’ ya pili ndani ya msimu huu wa 2022/2023 na ya kwanza jijini hapo, ‘Mbeya Derby’ inayozikutanisha Tanzania Prisons na Mbeya City.
Timu hizi zimekutana mara 14 kwenye michezo ya Ligi Kuu ambapo Tanzania Prisons wameshinda mara nne, Mbeya City wakishinda mara tatu huku wakienda sare michezo saba.
Mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana ilikuwa ni msimu wa 2015/2016 ambapo mchezo huu ulimalizika kwa Tanzania Prisons kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Katika michezo mitano ya mwisho ya Ligi Kuu timu hizi zilipokutana, Mbeya City wameonekana kuwa wababe kwa Tanzania Prisons, baada ya kuibuka na ushindi mara mbili na kwenda sare mara tatu.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu wa 2022/2023 Mbeya City wapo nafasi ya saba wakiwa na alama tatu huku Tanzania Prisons wakiwa nafasi ya tisa na alama zao tatu utofauti ukiwa katika mabao ya kufunga na kufungwa.