YANGA ‘YAIZIMA’ SINGIDA, MBEYA CITY, KAGERA HAKUNA MBABE.

IKIENDELEA kuonyesha ubabe baada ya kufuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika timu ya Yanga imeiadhibu Singida Big Stars mabao 4-1 katika mchezo wa mwisho wa kumaliza mzunguko wa 12 wa Ligi Kuu NBC.

Mchezo huo umeshuhudia mchezaji Fiston Mayele wa Yanga akiwa wa kwanza kufunga mabao matatu ‘Hat-trick’ katika Ligi Kuu NBC msimu huu huku bao lingine likifungwa na Kibwana Shomari dakika ya tatu baada ya kipindi cha pili kuanza.

Ushindi huu unaifanya Yanga kufikisha pointi 26 sawa na Azam huku Yanga akiongoza msimamo kwa tofauti ya mabao saba ya kufunga na kufungwa .

Mkoani Mbeya Klabu ya Mbeya City imelazimishwa sare ya mabao mawili dhidi ya Kagera Sugar ikiwa ni sare ya pili mfululizo katika uwanja wa nyumbani.

Bao la beki Hassan Muhamud raia wa Uganda dakika ya 85 akisawazisha mabao ya Anuary Jabir aliefunga dakika ya 18 na Mbaraka Yusuph dakika ya 48 limeipa alama moja timu ya Mbeya City huku bao lingine la timu hiyo likifungwa na Tariq Seif dakika ya 61.

Huu ni mchezo wa sita kwa Mbeya City bila kupoteza tangu septemba 13 walipofungwa na timu ya Azam kwa bao la Idris Mbombo.

Uwanja wa Highland Estate timu ya Ihefu imeshindwa kutamba nyumbani baada ya kuambulia kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa timu ya Polisi Tanzania.

Klabu ya Ihefu iliyotangulia kupata bao la kuongoza kupitia kwa Andrew Semchimba dakika ya 19 kipindi cha kwanza ilishindwa kuhimili mashambulizi ya Polisi waliopata bao la kusawazisha kupitia kwa Vitalisy Mayanga dakika ya 51 huku bao la ushindi likipatikana kupitia kwa Samwel Onditi aliejifunga dakika ya 78.

Mchezo huo wa tano kwa kocha Juma Mwambusi unaifanya Ihefu kuendelea kubaki mkiani katika msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi tano huku Polisi wakifikisha pointi tisa sawa na Dodoma Jiji huku maafande hao wakicheza mchezo mmoja zaidi ya Dodoma.

Ligi Kuu itaendelea tena Novemba 19 kwa michezo miwili Mbeya City itawakaribisha Geita Gold yenye pointi 17 sawa na Mbeya city huku Ruvu Shooting ikiikaribisha timu ya Simba katika uwanja wa Mkapa mkoani Dar es Salaam.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *