HAWA HAPA VINARA WA TAKWIMU LIGI KUU NBC.

MZUNGUKO wa 13 Ligi Kuu NBC unatarajiwa kuanza leo Novemba 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa mkoani Dar es Salaam kwa mchezo kati ya timu ya Ruvu Shooting na timu ya Simba majira ya saa 1:00 usiku.

Tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu wachezaji wamekua wakichuana katika takwimu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo za mwezi na mwisho wa msimu huu kwa vinara wa takwimu hizo.

Sixtus Sabilo wa timu ya Mbeya City anashikilia usukani katika orodha ya vinara wa mabao akiwa na mabao saba akifuatiwa na Idriss Mbombo(Azam), Moses Phiri(Simba), Fiston Mayele(Yanga) na Reliants Lusajo(Namungo) wenye mabao sita kila mmoja.

Takwimu za magolikipa zinaongozwa na Aishi Manula wa timu ya Simba mwenye michezo saba bila kuruhusu bao akifuatiwa na raia wawili kutoka Kisiwa cha Comoro Ally Ahamada wa Azam FC na Mahamoud Mroivil wa Coastal Union waliocheza mechi tano bila kuruhusu bao.

Wachezaji wenye pasi nyingi zilizozaa mabao wanaongozwa na Ayoub Lyanga wa timu ya Azam mwenye pasi tano sawa na Sixstus Sabilo wa Mbeya City wakifuatiwa na Saido Ntibazonkiza wa timu ya Geita Gold mwenye pasi nne za mabao.

Baada ya mchezo wa leo Ligi Kuu itaendelea tena kesho Novemba 20 kwa michezo mitatu, Ihefu wataikaribisha timu ya Coastal Union katika uwanja wa Sokoine majira ya saa 8:00 mchana huku Mbeya City wakiwakaribisha Geita Gold kwenye uwanja wa huo saa 10:00 alasiri baada ya mechi ya kwanza na mchezo wa mwisho utakaochezwa saa 1:00 usiku Namungo watakua nyumbani uwanja wa Majaliwa kujiuliza dhidi ya Azam FC.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *