AZAM YAENDELEA KUWA TISHIO

TIMU ya Azam imeendelea kuwa na mwenendo mzuri wa matokeo katika Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga timu ya Namungo bao moja ugenini na kufanikiwa kukusanya alama zote tatu zinazowapeleka nafasi ya kwanza katika msimamo.

Bao hilo limefungwa na beki Edward Manyama dakika ya 29 na kuendeleza rekodi bora ya kutokupoteza mchezo wowote kwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo Kali Ongala.

Matokeo hayo yanaifanya Namungo kusalia na pointi 15 katika nafasi ya tisa huku wakiwa na ukame wa kushinda katika michezo minne mfululizo.

Mkoani Mbeya mchezo wa mapema timu ya Mbeya City imetoka suluhu dhidi ya Geita Gold matokeo yanayofanya timu hizo kulingana Pointi 18 kila moja huku Mbeya City ikiwa na uwiano mzuri wa mabao.

Mchezo mwingine uliopigwa uwanja wa Highland Estates timu ya Ihefu imepata ushindi wa pili msimu huu baada ya kuifunga timu ya Coastal Union mabao 2-1.

Mabao ya Ihefu yamefungwa na Never Tigere dakika ya 42 na Niko Wadada dakika ya 46 huku bao pekee la Coastal likifungwa na Mbarack Amza dakika ya 38 linalomfanya kufikisha mabao matano katika orodha ya wafungaji msimu huu.

Pamoja na ushindi huo Ihefu wanaendelea kusalia nafasi ya mwisho katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na alama nane baada ya michezo 12.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *