BAADA ya kufunga mabao matatu ‘Hat-Trick’ katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Singida Big Stars mchezaji wa timu ya Yanga Fiston Mayele ameendelea kuwa mwiba kwa magolikipa baada ya kufunga magoli mawili leo dhidi ya Dodoma Jiji.
Mabao hayo yameisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa 2-0 na kuishusha timu ya Azam katika nafasi ya kwanza kwa tofauti ya mabao nane kwenye msimamo wa Ligi kwa kufikisha pointi 29 wakiwa na mechi tatu mkononi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Fiston Mayele aliyemaliza nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya George Mpole katika wafungaji kuongoza katika msimamo wa vinara wa mabao msimu huu.
Mchezo huo umeshuhudia Tuisila Kisinda na Dennis Nkane wakitoa pasi za mabao zao za kwanza tangu kuanza kwa msimu huu na mechi ya pili kwa golikipa Abutwalib Mshery bila kuruhusu bao.
Ligi kuu NBC itaendelea tena kesho Novemba 23 kwa michezo miwili kati ya Singida Big Stars na KMC uwanja wa Liti Singida majira ya saa 8:00 mchana huku Mbeya City watakua wenyeji wa Simba uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya saa 10:00 alasiri.