SIMBA YAENDELEA KUSOTA UGENINI

TIMU ya Simba imeendeleza rekodi mbaya katika Ligi Kuu NBC inapocheza michezo ya ugenini baada ya kushindwa kuondoka na pointi tatu katika uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya timu ya Mbeya City na kulazimishwa sare ya bao moja.

Simba wamecheza mechi sita ugenini na kufanikiwa kushinda mechi mbili pekee, kutoka sare tatu na kupoteza moja huku wapinzani wao wa jadi timu ya Yanga ikishinda mechi sita kati ya sita ilizocheza ugenini.

Mabao ya mchezo wa leo yamefungwa na Mzamiru Yassin dakika ya 15 kwa pasi ya John Bocco aliehusika katika mabao manne mpaka sasa katika mechi mbili mfululizo zilizopita huku bao la Mbeya City likifungwa na Tariq Seif dakika ya 79 kwa pasi ya Awadh Juma.

Baada ya kufanikiwa kupata alama moja timu ta Mbeya City imepanda mpaka nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi wakizidiwa alama mbili na timu ya Mtibwa Sugar pamoja na Singida Big Stars wenye pointi 21 huku simba ikisalia nafasi ya tatu na pointi 28.

Mkoani Singida timu ya Singida Big Stars baada ya kufungwa mabao 4-1 na timu ya Yanga mchezo wa raundi ya 12 leo imefanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC ya Dar es Salaam katika uwanja wa CCM Liti.

Singida ilijihakikishia ushindi kipindi cha kwanza dakika ya 40 kupitia kwa mchezaji wa zamani wa timu ya Simba aliewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa misimu miwili Meddie Kagere.

Ushindi wa leo unaifanya Singida kuendelea kushika nafasi ya nne wakifikisha pointi 21 na mchezo mmoja mkononi huku KMC ikisalia na pointi 14 katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.

Michezo miwili ya leo iliyopigwa mikoa ya Singida na Mbeya imekamilisha idadi ya michezo 100 tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu NBC.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *