TAARIFA KUTOKA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 25, 2022 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

 

Ligi Kuu ya NBC (NBCPL)

Mechi Namba 53: Singida Big Stars FC 1-1 Simba SC

Mchezaji wa timu ya Singida Big Stars, Shafiq Batambuze amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuingia kiwanjani kuanza kupasha moto misuli dakika 10 kabla ya muda ulioainishwa kwenye ratiba ya matukio ya mchezo.

Mchezaji huyo alipinga maelekezo ya Mratibu wa Mchezo (GC) na Kamishna wa Mchezo waliomtaka arejee chumbani hadi muda uliopangwa utakapowadia. Akiwa kiwanjani, Shafiq Batambuze alionekana kumwaga vitu kwenye majani jambo lililoashiria imani za kishirikina.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni 41:5(5.5) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Wachezaji.

 

Kamati imewafungia michezo mitatu na kuwatoza faini ya Sh. 1,000,00 (milioni moja) kila mmoja, Kocha Msaidizi wa Singida Big Stars, Mathias Lule na Kocha wa Makipa wa timu hiyo, Steven Kiagundu kwa kosa la kumuamuru Shafiq Batambuze aendelee kusalia kiwanjani hata pale mchezaji huyo alipojaribu kuondoka.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 45:2(2.4) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

 

Timu ya Singida Big Stars imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kushindwa kuhudhuria Mkutano wa Wanahabari uliopangwa kufanyika Novemba 8, 2022 kwenye ukumbi wa Benki ya NBC tawi la Singida, kuelekea mchezo tajwa hapo juu.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(56 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

 

Mechi Namba 94: Ihefu SC 1-2 Polisi Tanzania FC

Kamati imemfungia miezi mitatu (3) na kumtoza faini ya Sh. 500,000 (laki tano), Afisa Usalama wa klabu ya Polisi, Nelson Ngonyani kwa kosa la kumshambulia kwa matusi Mratibu wa Mchezo tajwa hapo juu, akipinga maelekezo halali yanayohusu kufuata taratibu za mchezo.

Afisa Usalama huyo aliendelea kwa kumtaka Mratibu wa Mchezo husika akashtaki kwenye mamlaka yoyote kwani anajua hakuna anayeweza kumfanya chochote.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 46:3 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

 

Mechi Namba 104: Dodoma Jiji FC 0-2 Young Africans SC

Timu ya Young Africans  imepewa onyo kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye Mkutano wa Wanahabari (Pre-Match Press Conference) kwa dakika 35.

Kocha Mkuu na nahodha au mchezaji mwenye ushawishi kikosini wanapaswa kushiriki mkutano wa Wanahabari siku moja kabla ya mchezo na katika muda uliopangwa kwenye ratiba ya mikutano hiyo.

Yanga walifika ukumbini saa 7:05 mchana badala ya saa 6:30 mchana.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(56 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Kamati imeionya timu ya Dodoma Jiji kwa kosa la viongozi wake kuingia katika chumba cha kuvalia wachezaji wa timu hiyo ndani ya muda wa kikanuni wa mchezo.

Viongozi hao walishuka kutoka jukwaani wakati wa mapumziko na kuingia ndani ya chumba hicho, kitendo ambacho ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:17 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:60 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

MUHIMU

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imepeleka mashauri yote ya waamuzi kwenye Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya uchambuzi wa kitaalamu wa maamuzi yote yenye utata yaliyofanyika kwenye michezo ya Ligi Kuu ya NBC, kabla ya kurejeshwa kwa ajili ya kujadiliwa na kutolewa maamuzi na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.

Ligi ya Championship

Mechi Namba 65: Biashara United FC 2-1 Kitayosce FC

Timu ya Biashara United imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake kutoa vitisho na lugha ya matusi kwa waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kabla ya kuanza kwa mchezo.

Mashabiki hao waliendelea kufanya vitendo visivyo vya kimchezo kwa kurusha mawe juu ya paa la chumba cha waamuzi wakitoa kauli za vitisho kuwa waamuzi hao wasingetoka salama uwanjani hapo kama timu yao isingepata matokeo ya ushindi katika mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

MUHIMU

Kamati imeitaka klabu ya Biashara United kuhakikisha vitendo vya namna hii havijirudii tena kwenye uwanja wao kwani vikijirudia, hatua kali zaidi za kikanuni zitachukuliwa ikiwemo kuzuia mashabiki kuingia uwanjani katika michezo yake yote au kuufungia uwanja Karume kutumika kwa michezo ya Ligi.

 

Mechi Namba 72: Gwambina FC 2-4 Ndanda FC

Klabu ya Gwambina imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 38.

Gwambina ilifika kwenye uwanja wa Nyamagana saa 9:08 alasiri badala ya saa 8:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:60 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Mechi Namba 73: Gwambina FC 2-1 Mashujaa FC

Klabu ya Gwambina imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 75.

Gwambina ilifika kwenye uwanja wa Nyamagana saa 9:45 alasiri badala ya saa 8:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:60 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 76: Mbuni FC 0-1 JKT Tanzania FC

Klabu ya Mbuni imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake wakiongozwa na Katibu wa klabu hiyo, Michael Yoen kuwashambulia waamuzi baada ya kumalizika kwa mchezo tajwa hapo juu kwenye uwanja wa Aga Khan jijini Arusha.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Kamati imemfungia miezi sita (6) na kumtoza faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) katibu wa Mbuni FC, Michael Yoen kwa kosa la kuongoza mashabiki kuwashambulia waamuzi na kuendelea kuwafuatilia waamuzi hao hadi hotelini walikofikia.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 46:3 ya Championship kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

 

Kamati imempongeza Afisa Usalama wa Chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Arusha (ARFA), Mike Warioba kwa juhudi zake za kuhakikisha waamuzi na Kamishna wa mchezo huo hawapati madhara zaidi kutokana na vurugu za mashabiki hao.

Mike Warioba aliwaondoa maafisa hao hotelini na kwenda kuwapa hifadhi katika kituo kikuu cha polisi Arusha kabla ya kuwatafutia usafiri wa kuwaondoa jijini Arusha usiku huo huo wa Novemba 19, 2022.

 

First League

Mechi Namba 14B: Stand United FC 2-0 Kasulu FC

Klabu ya Kasulu imepewa onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Kasulu iliwakilishwa na maafisa wawili (2) badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2(2.2) na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 19B: Kasulu FC 1-3 Rhino Rangers FC

Klabu ya Kasulu imepewa onyo kali kwa kosa la kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 80.

Kasulu ilifika kwenye uwanja wa Nyamagana saa 9:50 alasiri badala ya saa 8:30 mchana kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:(15 & 60) ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Kuhusu Klabu ya Njombe Mji

Bodi ya Ligi imepokea barua ya klabu ya Njombe Mji ya mkoani Njombe wakiomba kujitoa kushiriki First League msimu huu wa 2022/2023 baada ya na kukumbwa na matatizo ya kifedha, hali iliyosababisha timu hiyo ishindwe kumudu gharama za kushiriki ligi hiyo.

Kutokana na ombi hilo, Klabu ya Njombe Mji haitoendelea kushiriki First League msimu wa 2022/2023, imeshushwa daraja na kufungiwa kucheza Ligi kwa misimu miwili (2).

Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 31:4(4.1) ya First League kuhusu Kujitoa.

Kwasababu idadi ya michezo ambayo Njombe Mji imecheza hadi kujitoa kwake haizidi nusu ya michezo yote, matokeo ya michezo yote iliyocheza yamefutwa kwa mujibu wa Kanuni ya 31:4(4.3) ya First League kuhusu Kujitoa.

 

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Novemba 26, 2022

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *