IHEFU YAIZUIA YANGA KUENDELEA KUWEKA HISTORIA

Baada ya kucheza mechi 49 za Ligi bila kupoteza, hatimaye timu ya Yanga imefungwa na timu ya Ihefu mabao 2-1 huku Ihefu ikitoka nyuma na kusawazisha kisha kufunga bao la ushindi katika mchezo huo.

Yanga iliyokuwa na matokeo mazuri katika michezo ya ugenini kwa kucheza mechi sita na kushinda zote, leo imepoteza pointi tatu kwa mabao ya Never Tigere na Lenny Kisu huku bao lao pekee likifungwa na Yanick Bangala.

Mechi hiyo iliyopigwa uwanja wa Highland Estates imeshuhudia mashabiki wa Yanga wakitoka na huzuni baada ya mchezo huo uliokuwa wa kiporo kumalizika ukiwa ni mchezo wa kwanza kufungwa tangu Aprili 25 2021, walipofungwa na timu ya Azam.

Huu ni mchezo wa tatu kwa Ihefu kushinda na ukiwasaidia kutoka mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC na kupanda hadi nafasi ya 13 baada ya kufikisha pointi 11.

Licha ya matokeo hayo, bado timu ya Yanga inaendelea kusalia kileleni katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 32 huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi kutimiza idadi ya mechi 14.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *