MZUNGUKO wa 18 wa Ligi Kuu NBC umemalizika Desemba 26, kwa michezo mitatu iliyoshuhudia timu ya Simba ikipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC ugenini, Polisi Tanzania ikilazimishwa sare ya mabao 3-3 na Coastal Union huku Singida Big Stars ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.
Mzunguko huo umetamatika huku timu ya Yanga ikiendelea kuongoza katika msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 46 huku ikipoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya timu ya Ihefu na kutoka sare miwili dhidi ya Azam na Simba na kupoteza jumla ya pointi saba pekee mpaka sasa.
Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zinaongoza kwa kupoteza mechi nyingi (12) huku Polisi wakipoteza mechi tano nyumbani na saba ugenini na Ruvu wakipoteza mechi saba nyumbani na tano ugenini.
Timu ya Simba imekua kinara wa kufunga mabao (40) huku Zaidi ya nusu ya mabao hayo ikifunga katika viwanja vya ugenini (23) huku ikifuatiwa na timu ya Yanga iliyofunga jumla ya mabao (36) mpaka sasa.
Fiston Mayele wa Yanga ameendelea kuongoza msimamo wa wafungaji bora kwa kufikisha mabao 14 huku mabao 10 kati ya hayo akifunga kwa mguu wa kulia, mawili kwa kichwa na mawili kwa mguu wa kushoto akifuatiwa kwa karibu na Moses Phiri wa Simba mwenye mabao 10.
Mchezaji wa Simba Clatous Chama anaongoza kwa upande wa wachezaji wenye pasi nyingi zilizozaa mabao (10) akifuatiwa na Ayoub Lyanga wa Azam mwenye pasi saba huku beki wa Simba Mohammed Hussein akiwa beki mwenye pasi nyingi zilizozaa mabao akipiga pasi tano.
Ligi Kuu NBC itaendelea tena Desemba 30 kwa michezo mitatu itakayoshuhudia Singida Big Stars wakiikaribisha Geita Gold katika uwanja wa Liti, Simba SC itakua mwenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Benjamin Mkapa huku Dodoma Jiji ikiwa mwenyeji wa Kagera Sugar katika uwanja wa Jamuhuri, Dodoma.