SIMBA YAAGA MWAKA KIBABE, AZAM, YANGA KAMA KAWAIDA

MECHI kati ya Simba na Tanzania Prisons imeweka rekodi ya kuwa ya kwanza katika Ligi Kuu ya NBC kutoa wachezaji wawili tofauti waliofunga mabao matatu (Hat-Trick).

Mechi hiyo iliyochezwa Novemba 30, ilishuhudia wachezaji John Bocco na Saido Ntibazokinza wakifunga mabao matatu kila mmoja na kusaidia timu yao kushinda mabao 7-1 huku bao la saba likifungwa na beki Shomari Kapombe.

Mchezo huo ulishuhudia Prisons wakicheza kwa dakika 70 pungufu baada ya mchezaji wao Samson Mbangula kupewa adhabu ya kadi nyekundu dakika 20 iliyomfanya kushindwa kumaliza mchezo huo.

Wapinzani wakubwa wa timu ya Simba, timu ya Yanga imemaliza mwaka ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kushinda bao moja dhidi ya timu ya Mtibwa katika uwanja wa Manungu, Morogoro.

Bao pekee la timu ya Yanga limefungwa na Stephane Aziz Ki kwa mpira wa faulo akifikisha mabao manne huku mawili kati ya hayo yakifunga kwa faulo na kuwa mchezaji anayeongoza kwa magoli ya mipira iliyokufa.

Nayo timu ya Azam imemaliza mwaka kibabe kwa ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya timu ya Mbeya City ukiwa ushindi wao mkubwa kwa msimu huu.

Mabao ya Azam yamefungwa na Abdul Sopu aliyefunga mawili huku mengine yakifungwa na Prince Dube, Keneth Muguna, Iddy Nado, na Cleophas Mkandala.

Katika michezo mingine timu ya Singida BS imemaliza mwaka pia kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold na kusalia nafasi na nne na kufikisha pointi 37 kwa mabao ya Biemes Carno na Bruno Gomes aliyefunga kwa mkwaju wa penati huku bao pekee la Geita likifungwa na Haruna Shamte.

Mkoani Dodoma mabao ya Hassan Mwaterema na Collins Opare yalitosha kuifanya Dodoma kushinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na kumaliza mwaka ikiwa nafasi ya 12 ikiizidi Ihefu pointi nne.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena leo kabla ya kusimama kwa siku kumi kupisha mashindano ya kombe la Mapinduzi mpaka Januari 13, itakaporejea kwa mchezo kati ya Mtibwa Sugar na KMC kutoka Dar utakaopigwa katika uwanja wa Manungu, Morogoro.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *