YANGA YALIPA KISASI, AZAM IKITAMBA CHAMAZI

IKIWA timu pekee iliyoweza kuifunga Yanga katika msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa, Ihefu imeshindwa kurudia tena ilichokifanya kwenye duru la kwanza baada ya kukubali kipigo cha bao moja kutoka kwa vinara hao wa Ligi.

Ushindi huo kwa Yanga ni wa saba mfululizo tangu mara ya mwisho ilipopoteza mchezo wao dhidi ya Ihefu Novemba 29, 2022.

Bao hilo pekee limefungwa na Fiston Mayele anayeendelea kushika nafasi ya kwanza akiwa na mabao 15 katika msimamo wa vinara wa mabao Ligi Kuu ya NBC.

Baada ya ushindi huo Yanga inasalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya michezo 20 na kukusanya alama 53 huku Ihefu ikisalia nafasi ya 13 ikiwa na alama 20.

Kwenye uwanja wa Azam Complex timu ya Azam imeendelea kuzifanyia ubabe timu za Mbeya baada ya kuifunga timu ya Prisons mabao 3-0.

Katika mchezo huo imeshuhudiwa Abdul Sopu akifunga bao lake la tano msimu huu na kuendelea kutoa mchango wake tangu arejee kutoka katika majeruhi.

Mabao mengine ya timu ya Azam katika mchezo huo yamefungwa na Kipre Junior na Yona Amos aliejifunga na kuifanya Azam kufikisha mabao 36 msimu huu.

Ushindi huo umeifanya Azam kufikisha alama 43 ikizidiwa moja pekee na Simba inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *