SAIDO HAKAMATIKI LIGI KUU YA NBC.

AKICHEZA mchezo wake wa pili ndani ya kikosi cha Simba kiungo mshambuliaji raia wa Burundi Saido Ntibanzikiza ameendelea kuwa tishio kwa wapinzani baada jana kufunga mabao mawili na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City.

Mabao kwa upande wa Mbeya City yamefungwa na nyota wake, Richardson Ng’ondya na Juma Shemvuni wakitimiza idadi ya mabao 31 msimu huu kwa timu ya Mbeya City huku bao la tatu la Simba likifungwa na Pape Sakho.

Baada ya kufunga mabao hayo Saido amefikisha mabao tisa sawa na nahodha wa timu hiyo John Bocco wakizidiwa bao moja pekee na kinara Moses Phiri mwenye mabao 10 kwa wanaoongoza kwa mabao ndani ya kikosi cha Simba.

Kabla ya kuhamia timu ya Simba mchezaji huyo alifanikiwa kuifungia timu yake ya zamani Geita Gold mabao manne na kutoa pasi sita zilizozaa mabao kwa timu hiyo ya mkoani Geita.

Mpaka sasa Simba imeshinda michezo 14, sare mitano na kupoteza mmoja ikishika nafasi ya pili na pointi 47 nyuma ya Yanga iliyopo kileleni na pointi 53 huku Mbeya City katika michezo 20 ambayo imecheza imeshinda minne, sare tisa na kupoteza saba ikiwa nafasi ya 10 na pointi 21.

Duru la 21 Ligi Kuu ya NBC itaendelea tena kesho Januari 20, 2023 kwa michezo miwili itakayokutanisha timu za Kagera Sugar dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera huku timu ya Geita Gold ikiwa mwenyeji wa Polisi Tanzania katika uwanja wa Nyankumbu, Geita.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *