MSHAMBULIAJI wa timu ya Kagera Sugar Obrey Chirwa amejipata baada ya kuzidi kutupia mabao kwa kufikisha 17 hadi sasa ndani ya Ligi ya Championship ya NBC.
Ligi hiyo imeshachezwa mizunguko 28 huku ikiwa imesalia mizunguko miwili ili Ligi hiyo kufikia ukingoni ambapo pia mchezaji huyo ameisaidia timu yake kuwa nafasi ya pili kwenye msimamo huku ikipanda Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 68.
Maulid Shaban wa Geita Gold hayupo mbali akiwa amefanikiwa kuifungia mabao 16 timu yake ambayo ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC na imeshakata tiketi ya kucheza Ligi Kuu baada ya kukusanya alama 71.
Ramadhani Kalanje wa timu ya B19 nae ameweza kutikisa nyavu za wapinzani wao mara 13 huku timu hiyo ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo ikikusanya alama 34.
Abdereheman Mussa wa Transit Camp iliyopo nafasi ya tano kwenye msimamo na Emmanuel Mpuka wa Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya nne wameweza kufunga mabao 12 kila mmoja.
Adam Uledi aliyekuwa Transit Camp kabla ya kuhamia KMC ya Ligi Kuu ya NBC, Boniface Brown,Joseph Ambukege wa Mbeya Kwanza na Samson Kassian wa KenGold wamefanikiwa kufunga mabao 11 kila mmoja hadi sasa kwenye ligi hiyo.