Author: Honest Mwanitega

YANGA GEITA GOLD KUCHUANA KMC

LIGI Kuu ya NBC imeendelea kushika kasi ikiwa ni mzunguko wa sita wa ligi hiyo ambapo timu ya Yanga itaikaribisha timu ya Geita Gold katika uwanja wa KMC leo saa 1:00 usiku.

Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili ambazo zimeanza vema msimu zikipambana kupata alama muhimu mwanzoni ili kujiweka katika nafasi nzuri.

Timu ya Yanga ndio inashika nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi huku Geita Gold ikishika nafasi ya sita hivyo timu hizo zinatarajiwa kucheza kwa ushindani mkubwa ili kutopoteza alama za mchezo na kuendelea kushika nafasi nzuri zaidi.

Ikimbukwe kuwa Yanga imecheza michezo mitano na kushinda yote huku Geita Gold ikishinda michezo miwili, kusare mmoja na kupoteza miwili katika michezo mitano aliyoicheza ya ligi kuu ya NBC 2026/2027.

Katika mchezo wa mwisho Yanga amepata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Fountain Gate huku Geita Gold akipoteza kwa mabao mawili kwa sifuri katika mchezo wake na Simba.

MBIO ZA UBINGWA WA LIGI KUU YA NBC ZIMEANZA ‘ASUBUHI’

Mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27 zimeanza mapema kwa kasi huku wapinzani wa jadi timu za Young Africans (Yanga) na Simba, zikionyesha mapema kuwa huenda tena wakawa wahusika wakuu katika vita ya kutwaa taji la ligi msimu huu.

Hadi sasa, baada ya kila timu kucheza michezo mitano, Yanga na Simba zimekusanya alama 15 kila mmoja, zikiwa zimeshinda michezo yote mitano ya mwanzo huku tofauti kati yao ikiwa kwenye mabao ambapo Yanga ikifunga mabao 15 huku Simba ikiwa imefunga tisa ,jambo linalowafanya mabingwa watetezi Yanga kushika nafasi ya kwanza.

Yanga na Simba zimekuwa na mwanzo wa kuvutia kwenye eneo la ulinzi zikiruhusu mabao mawili pekee ambapo timu hizo zinaongozwa na manahodha wao kwenye eneo hilo, Rushine De Reuck akiwa Simba na Bakari Mwamnyeto akiwa Yanga.

Hii ina maana kwamba, katika hatua hii ya mwanzo wa msimu, hakuna hata mmoja kati ya ‘watani’ hawa aliyeko tayari kupoteza mchezo wowote huku pia timu hizo zikiiwakilisha nchi kwenye Kombe la Mabingwa Afrika.

Kwa miaka mingi, pambano la Simba na Yanga limekuwa zaidi ya mechi mbili wanapokutana uwanjani. Ni pambano linaloendelea katika kila mchezo wa msimu, ambapo ushindi wa Yanga unakuwa presha kwa Simba kushinda mechi yake inayofuata, na ushindi wa Simba unaiweka Yanga kwenye wajibu wa kujibu.

Libasse Gueye wa Simba ameendelea kuwa muhimili wa Simba kwenye eneo la ushambuliaji akiwa amefunga bao moja na kutoa pasi za mabao tano huku usajili mpya wa Yanga Peter Shalulile akiwa kinara baada ya kufunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa uwanja wa Jamhuri, Dodoma kati ya Dodoma Jiji na Namungo timu hizo zikiwa zimepishana kwa alama moja pekee ambapo Dodoma imekusanya alama saba na Namungo alama sita.

PAZIA LA LIGI KUU YA NBC 2026/27 LAFUNGULIWA KIBABE.

Msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC umeanza kwa ushindani mkali, mabao na matokeo yaliyotoa picha ya namna safari ya msimu wa 2026/27 inavyotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Mchezo wa ufunguzi wa msimu uliwakutanisha Pamba Jiji na Dodoma Jiji kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na lushuhudia timu hizo zikitoshana nguvu kwa sare ya 1-1.

Dodoma Jiji ndiyo ilianza kupata bao kupitia Beno Ngassa ambaye kwa kufunga kwake aliweka historia ya kuwa mfungaji wa bao la kwanza la msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC.

Pamba Jiji haikukubali kukaa nyuma na ilifanikiwa kurejea mchezoni kupitia Deogratius Mafie aliyefunga bao la kusawazisha na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa alama kugawanywa.

Katika mchezo mwingine mabingwa wa NBC Championship msimu uliopia timu ya Geita Gold ilianza msimu kwa ushindi muhimu wa ugenini baada ya kuichapa Mbeya City 1-0 katika Uwanja wa Sokoine.

Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Obrey Chirwa aliyekuwa shujaa wa Geita Gold kwa kuipa timu yake alama tatu katika mechi ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa.

Ushindi huo umeipa Geita Gold mwanzo mzuri wa msimu huku Mbeya City ikilazimika kusubiri mchezo mwingine kutafuta alama zake za kwanza.

Kwenye mchezo wa mwisho, Singida ilitoa  kipigo cha nguvu baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Fountain Gate.

Singida ilipata mabao yake kupitia Jonathan Sowah, Yusuph Adam na Mathew Tegisi na kupata matokeo yaliyoiweka kwenye nafasi nzuri katika mwanzo wa msimu.

Ushindi wa mabao matatu bila jibu umeifanya Singida kuonyesha mapema kuwa haijaingia kwenye msimu huu kwa ajili ya kushiriki pekee, bali ipo tayari kupigania matokeo na nafasi za juu.

Aafari ikiwa ndiyo kwanza imeanza, macho sasa yanaelekezwa kwenye michezo inayofuata kuona ni timu gani itaendelea na kasi yake na ni wachezaji gani watainuka kuwa mastaa wa msimu mpya.

MZUNGUKO WA 23 WATAMATIKA KIBABE LIGI KUU YA NBC.

LIGI Kuu ya NBC jana ilitoa burudani ya kiwango cha juu huku mashabiki wakishuhudia jumla ya mabao 13 yakifungwa kwenye viwanja tofauti.

Mchezo wa mapema kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya uliwakutanisha ‘Maafande’ wa Tanzania Prisons waliopata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya.

George Mpole aliibeba timu hiyo kwa bao lake la dakika ya 26 lililowapa furaha mashabiki wa nyumbani huku Fountain ikipambana kusawazisha lakini ukuta wa Prisons ulikuwa imara mpaka filimbi ya mwisho.

Mchezo mwingine wa mapema uliotikisa zaidi jana ulikuwa kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya KMC ambapo mashabiki walishuhudia tamasha la mabao saba baada ya Mtibwa kuibuka na ushindi wa 4-3 kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Magata Fredrick alianza mapema dakika ya 30 kabla ya Oscar Masai, Said Mkopi na Kassimu Msafiri kuongeza mabao mengine yaliyowapa ushindi muhimu huku kwa upande wa KMC, Daruweshi Saliboko alipachika mawili na Rashid Chambo akiingia kwenye orodha ya wafungaji ingawa juhudi zao hazikutosha kuzuia kipigo hicho.

Kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma timu ya Simba imeendelea kuonyesha makali yake baada ya kuichapa Mashujaa mabao 3-0 kwenye mchezo uliokuwa na ‘presha’ kubwa.

Nahodha Clatous Chama alikuwa nyota wa mchezo huo baada ya kufunga mabao mawili dakika za 6 na 79 kabla ya Seleman Mwalimu aliyeingia kipindi cha pili kuweka msumari wa mwisho dakika ya 90+2.

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha alama 52 na kuendelea kuweka presha kubwa kwenye mbio za ubingwa wakiwasogelea kwa karibu wapinzani wao wakubwa Young Africans waliopoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Dodoma Jiji waliokusanya alama 54.

Mchezo wa mwisho ulishuhudia Azam ikipata ushindi wa dakika za mwisho baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Pamba Jiji ya Mwanza.

Feisal Salum aliipatia Azam bao la kwanza dakika ya 90 linalomfanya kufikisha mabao 11 na kuendelea kuwa kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu ya NBC hadi sasa huku bao la pili likifungwa na Jephte Kitambala.

Matokeo hayo yanaendelea kuongeza moto kwenye msimamo wa ligi huku kila timu ikipigania malengo yake kama vile ubingwa, nafasi za kimataifa na kujiokoa kutoka kwenye mstari wa kushuka daraja.

WIKI YA MAAMUZI, KUTOKA NEW AMAAN HADI MEJ. JEN ISAMUHYO.

SAFARI inaanza Aprili 29, visiwani Zanzibar ambapo macho yote yataelekezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex timu za Simba na Young Africans (Yanga) zitakapokutana katika fainali ya Kombe la Muungano kwenye mchezo wenye uzito wa kipekee unaobeba heshima ya kitaifa na hadhi ya ushindani wa kihistoria kati ya timu hizi mbili.

Fainali hii si tu pambano la kutwaa taji, bali ni kipimo cha nguvu, mbinu na utayari wa kila kikosi kuelekea mechi nyingine kubwa zaidi inayofuata ya Ligi Kuu ya NBC timu hizo zitakapokutana.

Ndani ya dakika 90 (au zaidi), mshindi atajipatia faida ya kisaikolojia itakayoweza kuathiri moja kwa moja matokeo ya Kariakoo derby ya Mei 3 kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam unaotumiwa na timu ya Simba.

Kabla ya Kariakoo Derby ya Mei 3 ndani ya Dar es Salaam, hali ya msimamo wa Ligi Kuu ya NBC inaipa hadithi hii uzito wa kipekee kuelekea mchezo huo ambapo Yanga wanaongoza wakiwa na rekodi ya kuvutia.

‘Wananchi’ wamecheza michezo 19 bila kupoteza wakishinda 14, sare tano, mabao 44 ya kufunga na mabao matatu tu ya kufungwa huku ikikusanya alama 47 hadi sasa.

Kwa upande wa ‘Mnyama’ ameshinda 12, sare sita, ‘kichapo’ kimoja dhidi ya Azam, mabao 32 ya kufunga na saba ya kuruhusu huku ikikusanya jumla ya alama 42 hadi sasa.

Takwimu hizi zinaonyesha tofauti ndogo sana kwa ‘miamba’ hii inayotikisa Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku Yanga wakionekana kuwa na uimara mkubwa hasa kwenye safu ya ulinzi na Simba wakibaki kuwa tishio lenye uwezo wa kubadilisha mchezo kwa haraka kwenye safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Selemani Mwalimu.

Katika upande wa ushambuliaji, Yanga wanaonekana kuwa na mgawanyo mpana wa mabao, hali inayowafanya kuwa vigumu kuzuilika huku wachezaji wao Prince Dube raia wa Zimbabwe akifunga mabao nane, Pacome Zouzoua wa Ivory Coast akifunga saba na Mudathir Yahya raia wa Tanzania akifunga saba huku akitarajiwa kukosa mchezo huo wa jumapili kutokana na adhabu aliyopewa ya kufungiwa baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji Ibrahim Abraham.

Kwa upande wa ‘Mnyama’ mchezaji wa Wydad Casablanca ya Morocco raia wa Tanzania anayekipiga kwenye timu hiyo kwa mkopo Selemani Mwalimu hadi sasa amefunga mabao 6 huku Libasse Gueye wa Senegal akifunga manne akiwa na mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba hadi sasa sambamba na Anicet Oura wa Ivory Coast aliyesajiliwa dirisha dogo la msimu huu.

Hii inaonyesha tofauti ya kimkakati ambapo Yanga wakitegemea mfumo wa timu nzima kushambulia, huku Simba wakitumia ufanisi na nidhamu ya kiufundi kupata matokeo ya ushindi.

Kwa miaka ya hivi karibuni, rekodi ya Kariakoo Derby imekuwa na ushindani mkali, lakini takwimu zinaipa Yanga nafasi ya kujiamini zaidi kutokana na mfululizo wa matokeo mazuri wanayopata wakikutana na wapinzani wao hao wa Kariakoo.

Hata hivyo, derby ina tabia ya kuvunja hesabu zote ndani ya dakika 90 ambapo historia inaweza kufutwa na kuandikwa upya kutokana na maandalizi na ufanisi wa kutumia nafasi kwa timu zote mbili.

Kinachofanya ratiba hii kuwa ya kipekee si tu ukubwa wa mechi, bali ukaribu wake kwani fainali ya Muungano inakuja siku chache kabla ya dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu ya NBC hali inayobadilisha kabisa maandalizi ya timu zote mbili.

Mshindi wa Zanzibar ataingia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC akiwa na morali ya juu na ataweka presha kwa mpinzani kuelekea mchezo wa ligi huku anayeshindwa ataingia na hasira na atajaribu kulipiza kisasi hali inayofanya kuongeza joto la michezo hiyo hivyo basi mechi hizi mbili si matukio tofauti bali ni sura mbili za simulizi moja.

Kutoka visiwa vya Zanzibar hadi mitaa ya Kariakoo, Tanzania inajiandaa kushuhudia burudani ya kiwango cha juu, presha isiyo na mfano na historia mpya ikiandikwa kwa michezo miwili ya Kariakoo Derby kupigwa ndani ya wiki moja.

Swali linabaki kuwa moja tu:
Nani ataibuka kuwa mfalme wa wiki hii kati ya Simba au Yanga?