BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inatangaza mabadiliko ya tarehe ya kurejea kwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC ambayo hapo awali ilipangwa kuendelea Machi 1, 2025 baada ya kutamatika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi na fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Michezo ya Ligi Kuu ya NBC itarejea katika juma la kwanza la Februari, 2025 kwa michezo ya ‘viporo’ kabla ya kuendelea na michezo ya mzunguko wa 17. Tarehe rasmi pamoja na ratiba iliyofanyiwa maboresho, zitatangazwa hivi karibuni.
Mabadiliko hayo yamekuja baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kusogeza mbele fainali za CHAN kutoka Februari 1, 2025 hadi Agosti, 2025 hivyo kutoa nafasi kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kuendelea na michezo ya Ligi Kuu ya NBC ambayo ilisimama kupisha fainali hizo.
Bodi ya Ligi inatoa wito kwa klabu zote kuhakikisha zinaongeza nguvu katika maandalizi ya timu zao kiufundi pamoja na masuala mengine hasa yahusuyo miundombinu ya viwanja, ambavyo vitakaguliwa kabla ya kurejea kwa Ligi.
Viwanja vitakavyonekana kukosa sifa vitaondolewa katika orodha na klabu mwenyeji italazimika kuteua uwanja mwingine miongoni mwa vilivyothibitishwa, kwa ajili ya michezo yake ya nyumbani.
Bodi inazitakia kila la kheri klabu zote na wadau wengine katika maandalizi yao kuelekea kurejea kwa Ligi Kuu ya NBC.