Category: Uncategorized

AZAM KUISHUSHA YANGA KILELENI LEO?

 

MZUNGUKO wa 12 wa Ligi Kuu NBC unatarajia kuanza leo Novemba 15,kwa michezo miwili itakayopigwa mkoani Dar es Salaam katika viwanja vya Uhuru na Azam Complex.

Mchezo wa saa 10 alasiri utakaochezwa uwanja wa Uhuru KMC watakua wenyeji wa Dodoma Jiji iliyopoteza mchezo dhidi ya Azam huku kwenye uwanja wa Azam Complex timu ya Azam itaikaribisha Ruvu Shooting ya mkoani Pwani.

Azam inaelekea katika mchezo wake ikiwa katika fomu nzuri ya kupata alama tatu kwenye kila mchezo chini ya Kaimu kocha mkuu Kali Ongala baada ya kushinda katika michezo minne mfululizo dhidi ya Simba,Ihefu,Dodoma Jiji na Mtibwa na kufikisha alama 23 sawa na vinara wa msimamo Yanga.

“Jambo muhimu kwetu kwa sasa ni kupata alama tatu muhimu katika kila mchezo kwani kila mechi ya ligi kuu ni mgumu kutokana na kila timu kuwa na maandalizi ya kushindana”alisema Kali.

Naye kocha msaidizi wa Ruvu Shooting Rajab Mohammed amesema kuwa timu yake imejiandaa vizuri na wamefanyia marekebisho makosa yote yaliyojitokeza michezo ya nyuma hivyo wanaamini wataenda kupata matokeo chanya dhidi katika mchezo wa leo.

“Azam ni timu bora iliyokamilika kila idara,tumeawaona ubora na madhaifu yao na tumewaelekeza vijana namna ya kucheza dhidi yao hivyo tunaamini tutapata matokeo chanya katika mchezo wetu dhidi yao.”alisema Rajab.

HOTUBA YA MWENYEKITI – BODI YA LIGI KUU TANZANIA MKUTANO WA TISA WA BARAZA KUU LA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

 

Ndugu Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo;

Ndugu Ally Mayay, Mkurugenzi wa Michezo;

Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania;

Wenyeviti Klabu za Ligi Kuu;

Wenyeviti Klabu za Championship;

Wenyeviti Klabu Za First League;

Ndugu Wilfred Kidao, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania

Ndugu Almasi Jumapili Kasongo, Afisa Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi Kuu Tanzania,

Wenyeviti wa Vyama Vishiriki (FRAT, TAFCA, TASMA, SPUTANZA na TWFA);

Mwakilishi wa Kamati ya Maadili ya TFF (Amin Bakhressa)

Wakurugenzi wote wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania;

Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji;

Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu Tanzania, NBC Bank Limited;

Wadhamini wenye haki za Matangazo ya Runinga, Azam Media Limited;

Wadhamini wenye haki za Matangazo ya Radio, Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC);

Sekretariati ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania;

Ndugu Wenyeviti na Wajumbe wa Mkutano Mkuu;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana,

Ni matumaini yangu kuwa muwazima wa afya na mnaendelea vizuri na shughuli za kila siku za maendeleo na ukuaji wa mpira wa miguu katika nchi yetu.

Rambirambi za kina ziwafikie Marafiki na Familia za Wanamichezo wote waliopoteza wapendwa wao katika kipindi cha ndani ya mwaka mmoja nchini Tanzania na Duniani kwa ujumla wake.

Lakini pia nawaomba tusimame kwa dakika moja kuwaombea wenzetu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege ya Kampuni ya Precision iliyotokea mkoani Kagera Novemba 6, 2022.

Bodi imeendelea kufanya vizuri tangu tulipokutana kwa mara ya mwisho kwenye Mkutano Mkuu wa kawaida na Uchaguzi uliofanyika Cate Hotels, Morogoro na kuendelea kuweka msingi imara wa ushindani kwa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla wake, lengo kuu likiwa ni kuona kwa namna gani klabu zetu zinaweza kuwa bora na zinaingia kwenye orodha ya klabu 10 bora barani Afrika.

Sisi sote ni mashuhuda kwa mara nyingine tena ligi yetu imeweza kuwa miongoni mwa ligi kumi (10) bora barani Afrika na ligi ya 62 Duniani. Lakini pia tumeweza kutoa uwakilishi wa klabu nne kwenye mashindano ya Klabu Bingwa na Shirikisho Afrika.

Bodi imeendelea na dhamira ya kuhakikisha kwamba michezo yetu yote ya Ligi inachezwa katika viwanja vinavyokidhi matakwa ya KIKANUNI na SHERIA namba moja (UWANJA) katika sheria 17 za mpira wa miguu lakini vinavyokidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika na Duniani (FIFA).

Msingi wake mkubwa ukiwa ni upatikanaji wa HAKI na mechi kuchezwa kwenye viwanja vilivyo salama kwa mazingatio ya ulinzi wa wachezaji na watazamaji kwa ujumla wake kama ambavyo CAF na FIFA wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na viwanja bora na salama kwa nyakati zote.

Lakini pia napenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole sana Wenyeviti wenzangu pamoja nami binafsi kwa viwanja vyetu kufungiwa kutumika kwa michezo ya ligi mpaka pale maboresho yatakapofanyika ili kukidhi matakwa ya Kanuni na Sheria za mpira wa miguu. Kwa taarifa niliyonayo viwanja vingi vilivyokuwa vimefungiwa sasa vimefunguliwa na vinaendelea na matumizi yake kama kawaida isipokuwa viwanja vya Jamhuri (Dodoma) na Mabatini (Pwani) vinavyotumiwa na Dodoma Jiji na Ruvu Shooting kwa mfuatano.

Bodi kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tumeendelea kuimarisha eneo la UAMUZI na WAAMUZI kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali kupitia wakufunzi wa ndani na nje ya nchi ambao wanatambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Duniani (FIFA).

Mijadala na mipango mbalimbali ya namna gani ya kuimarisha eneo la UAMUZI na WAAMUZI imeendelea na lengo ni kuona UHURU, UADILIFU, HESHIMA na UAMINIFU kwa UAMUZI na WAAMUZI yanakuwa kipaumbele cha kwanza kwa MWAMUZI na bila kumsahau KAMISAA kwa wakati wote.

Pamoja na   juhudi zote hizo, tunakiri kuwa eneo la uamuzi limeendelea kuwa na changamoto katika kutafsiri sheria 17 za mpira wa miguu. Lakini pamoja na juhudi kubwa tunazofanya kuhusiana na kuondoa changamoto tulizokuwa nazo ndugu Wenyeviti wenzangu na wajumbe wa Mkutano Mkuu ni ukweli usiopingika kwamba matumizi ya Teknolojia (VAR, Goal line technology na Communication tools) yamekuwa ni kitu cha MUHIMU na LAZIMA katika kuwasaidia waamuzi wanapokuwa kwenye majukumu yao ya kutafsiri Sheria 17 za mpira wa miguu.

Bodi inaamini kuwa huu ni wakati sahihi wa kuanza kutumia TEKNOLOJIA tajwa hapo juu.

Bodi kwa kushirikiana na TFF tumejielekeza kwenye utekelezaji wa masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations) kwa asilimia 100 kama tulivyokubaliana na kuazimia kwenye Mkutano Mkuu wa Klabu uliofanyika Desemba 15, 2020 tukiamini kuwa utekelezaji wa Kanuni tajwa hapo juu ndiyo dawa pekee ya kuondoa changamoto nyingi tulizokuwa nazo kwenye mpira wa miguu.

Utekelezaji wa Kanuni ya Leseni ya Klabu ni moja ya vipaumbele vyangu vikuu katika kuhakikisha ligi zetu na mpira wa miguu kwa ujumla wake unapiga hatua. Hivyo basi ni matarajio yangu kuwa utekelezaji wa Kanuni ya Leseni za Klabu tutausimamia na kuuchukulia kwa uzito mkubwa ili uweze kuja kutusaidia kuondoa changamoto nyingi tulizokuwa nazo katika usimamizi na uendeshaji wa ligi.

Mafanikio na ukuaji wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kwa kiasi kikubwa unategemea mafanikio na ukuaji wa klabu zetu hivyo basi ili tuweze kufikia mafanikio hayo Bodi, Klabu, Vyama vishiriki vya mpira wa miguu (FRAT, TAFCA, TASMA, SPUTANZA na TWFA), vyama vya mpira wa miguu vya mikoa/wilaya hatuna budi kuajiri wafanyakazi wenye uzoefu na sifa katika nafasi wanazozifanyia kazi ili tuweze kuleta tija katika taasisi zetu.

Bodi itaendelea kusimamia na kuboresha mahusiano na wadau wake wote klabu, vyama vishiriki, vyama vya mpira wa miguu vya Mikoa/Wilaya, Wadhamini, Wamiliki wa Viwanja, Kampuni/Mashirika, Vyombo vya habari, Waandishi, Mashabiki bila kusahau mdau mkubwa na namba moja, Serikali.

Kupungua kwa idadi ya watu wanaoingia viwanjani kutazama mechi za ligi zetu hasa Ligi Kuu ni eneo jingine muhimu ambalo Bodi tumeanza kulifanyia kazi kwa umakini mkubwa ili tuweze kupata njia mbadala ya kurejesha watu viwanjani kama ilivyokuwa katika siku za nyuma.

Hivyo basi nawaomba Wenyeviti wote tujifikirishe namna ya kutafuta njia bora ya kufanya ili tuweze kuleta watu viwanjani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika Mikoa yetu. Rejea taarifa ya mapato na mashabiki walioingia uwanjani kwa kila timu msimu 2021/2022.

Rasilimali fedha kimeendelea kuwa kipaumbele cha kwanza katika kutimiza majukumu ya Bodi na Klabu zetu. Ni matarajio yangu kuwa kuimarika kwa eneo la rasilimali fedha ni kuimarika kwa usimamizi, uendeshaji na utekelezaji wa majukumu ya Bodi na klabu kwa ujumla. Hivyo basi katika kipindi changu cha uongozi nitaendelea kuhakikisha Ligi zetu zote zinakuwa na wafadhili wengi iwezekanavyo ili kuweza kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea.

Lakini naomba nichukue nafasi hii kuwaomba Wenyeviti wenzangu tuweze kuajiri watu wa masoko wazoefu na wenye sifa katika Klabu zetu ili tuweze kuondokana na changamoto ya Rasilimali Fedha.

Napenda kuwaasa Wenyeviti wenzangu kuweza kusimamia na kutekeleza Kanuni za Ligi zetu zote tatu kama zilivyopitishwa. Kumekuwa na changamoto kubwa kwa Klabu kutozingatia na kuheshimu Kanuni za Ligi jambo linalosababisha uwepo wa matukio mengi yasiyo ya kimichezo na yanayochafua taswira ya Ligi zetu lakini matukio hayo yamekuwa yakisababisha Klabu ziadhibiwe mara kwa mara kwa kutozwa faini ama viongozi/wachezaji kufungiwa kwa mujibu wa Kanuni.

Ni matarajio yangu baada ya Mkutano huu Wenyeviti tutarudi kwenye klabu zetu na kuona namna gani tunaweza kuelimishana na kusimamia kanuni tulizojiwekea.

Nina hakika kwamba msingi imara na maendeleo mazuri tuliyopata tangu tukutane kwa mara ya mwisho katika Mkutano Mkuu uliofanyika Cate Hotels, Morogoro, muda si mrefu ligi zetu na mpira nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla zitakuwa na ushindani zaidi na kuvutia kwa Mashabiki, Wafadhili na Wadau wengine wa Mpira wa Miguu Duniani kote.

Mwisho tunatambua nguvu ya kipekee ya mpira wa miguu katika Kuwaunganisha watu wa jinsia zote, rika zote, kabila, dini na tamaduni mbalimbali katika nchi yetu. Hivyo basi tutambue tuna jukumu la kuendelea kuwaunganisha watanzania na Afrika kwa ujumla kupitia malengo yetu makuu ya kuhakikisha ligi zetu zote tatu tunazisimamia kwa uweledi na ufanisi mkubwa.

Pamoja Tunaweza.

Ahsanteni Sana.

Steven J. Mnguto

MWENYEKITI – TPLB

SINGIDA,SIMBA ZATOSHANA NGUVU,AZAM YAPETA

TIMU za Singida Big Stars ya mkoani Singida na Simba SC ya Dar es Salaam zimeshindwa kutambiana kwenye uwanja wa CCM Liti baada ya kutoka sare ya bao moja.

Katikati ya watazamaji Zaidi ya elfu 11 waliofurika uwanjani kutazama mchezo huo wa Ligi Kuu NBC, Singida ilikuwa ya kwanza kupata bao lililowapeleka mapumziko kifua mbele kupitia kwa Deus Kaseke dakika ya 11, akiunganisha krosi ya mchezaji wa zamani wa Simba, Said Ndemla.

Simba walipata bao lao la kusawazisha dakika ya 58 kupitia kwa Peter Banda aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Jonas Mkude.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha alama 18 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo sawa na Singida waliopo nafasi ya tatu wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC imepata ushindi wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga timu ya Dodoma Jiji mabao 2-1 kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam katika mchezo huo yamefungwa na Ismael Aziz Kader dakika ya 37 na Idris Mbombo dakika ya 89 huku bao pekee la Dodoma likifungwa na Collins Opare dakika 41.

Matokeo hayo yanaifanya Azam kufikisha alama 20 sawa na vinara wa Ligi Yanga wakitofautiana kwa magoli ya kufunga na kufungwa huku Dodoma ikisalia na alama sita katika nafasi ya 14 ya msimamo wa ligi ya NBC.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena Novemba 10 katika uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya kwa mchezo kati ya Tanzania Prisons na Coastal Union ya Tanga.

TAARIFA KUTOKA BODI YA LIGI KUU TANZANIA

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Novemba 4, 2022 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kufanya maamuzi yafuatayo;

 

Ligi Kuu ya NBC (NBCPL)

Mechi Namba 64: Young Africans SC 1-1 Simba SC

Timu ya Young Africans imetozwa faini ya Sh. 5,000,000 (milioni tano) kwa kosa la kuingia chumba cha kuvalia kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo tajwa hapo juu uliofanyika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Oktoba 23, 2022.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:(21 & 60) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mchezaji wa timu ya Young Africans, Stephan Aziz Ki na Clatous Chama wa klabu ya Simba wamefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kukwepa kusalimiana na wachezaji wa timu pinzani kabla ya kuanza kwa mchezo tajwa hapo.

Wachezaji hao kwa nyakati na mazingira tofauti walionekana kufanya hila kwa kusubiri nje ya kiwanja ili kusubiri zoezi la kusalimiana likamilike ndipo waingie kiwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni 41:5(5.4) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa Wachezaji.

 

Mashabiki na Wanachama wa klabu ya Yanga, Israel Suma, Kais Mwasongwe, Soud ‘Tall’ na Mohamed Mposo wamefungiwa miezi mitatu (3) kwa kosa la kuwavamia waamuzi wa mchezo tajwa hapo juu wakiwa wanaelekea chumbani wakati wa mapumziko, kabla walinzi wa uwanjani (Stewards) hawajaingilia kati na kuwaondoa.

Mashabiki na wanachama hao ambao wanatumiwa na klabu ya Young Africans kama maafisa wasaidizi wa usalama, walionekana kupitia picha jongeo (video) zilizonaswa na kamera za uwanja wa Benjamin Mkapa, wakifanya kitendo hicho wakiwa katika njia ya kuelekea vyumba vya kuvalia.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:2 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

Mechi Namba 74: Geita Gold FC 0-1 Young Africans SC

Mwamuzi wa kati, Florentina Zabron amepelekwa Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za mpira wa miguu katika mchezo tajwa hapo juu.

Kamati ya Waamuzi ya TFF italitazama kitaalamu tukio la pigo la penati ya klabu ya Young Africans dhidi ya Geita Gold katika dakika ya 18 ya mchezo kabla ya kuishauri Kamati kwa kuzingatia kanuni ya 42:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti Waamuzi.

 

Ligi ya Championship

Mechi Namba 46: Pamba FC 1-0 Pan African FC

Timu ya Pan African imepewa onyo kwa kosa la kuchelewa kuwasili kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo (MCM) kwa dakika tano (5) huku pia ikichelewa kwenye chumba chao cha kuvalia wakati wa mapumziko jambo lililosababisha kipindi cha pili cha mchezo tajwa hapo juu kichelewe kuanza kwa dakika tano (5).

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 17:2(2.2) na 17:(33 & 60) ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 55: Fountain Gate FC 1-0 Ndanda FC

Klabu ya Fountain Gate imetozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la mashabiki wake kwenda kusimama nyuma ya goli la klabu ya Ndanda na kuanza kumtolea lugha za matusi golikipa wa timu hiyo wakimshutumu kuwa ameweka kitu golini ambacho kinazuia Fountain Gate kupata ushindi.

Mashabiki hao walimshinikiza mtoto muokota mipira (ball kid) kwenda golini na kuchukua chupa ya maji ya golikipa huyo kisha kuitupa nje.

Adhabu hiyo ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

 

First League

Mechi Namba 6B: Mbao FC 1-1 Mwadui FC

Klabu za Mbao na Mwadui zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Mbao waliwakilishwa na maafisa wanne (4) huku Mwadui wakiwakilishwa na maafisa wawili (2) badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Katika kikao hicho, Mwadui walikuwa na seti moja ya jezi za wachezaji wa ndani bila jezi za magolikipa wala soksi.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2(2.2) na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Kamati imemfungia michezo mitatu (3) mtunza vifaa wa klabu ya Mbao, Bw. Chriss Shimbe baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo tajwa hapo juu kwa kosa la kurudia mara kadhaa kupinga maamuzi ya waamuzi wa mchezo huo.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 47:21 ya First League kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.

 

Mechi Namba 6B: Cosmopolitan FC vs Majimaji FC

Klabu ya Cosmopolitan imepewa ushindi wa alama tatu (3) na mabao matatu (3) huku klabu ya Majimaji ikitozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) na kupokwa alama 15 katika msimamo wa Ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandaalizi ya mchezo na baadae uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu.

Maafisa wa mchezo huo walisubiri kwa dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Majimaji kutoonekana uwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1(1.6) ya First League kuhusu Kutofika Uwanjani.

 

Mechi Namba 10A: African Lyon FC vs Njombe Mji FC

Klabu ya African Lyon imepewa ushindi wa alama tatu (3) na mabao matatu (3) huku klabu ya Njombe Mji ikitozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) na kupokwa alama 15 katika msimamo wa Ligi kwa kosa la kushindwa kufika kwenye kikao cha maandaalizi ya mchezo na baadae uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo tajwa hapo juu.

Maafisa wa mchezo huo walisubiri kwa dakika 30 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni kabla ya kuahirisha mchezo huo baada ya klabu ya Njombe Mji kutoonekana uwanjani.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 31:1(1.6) ya First League kuhusu Kutofika Uwanjani.

Mechi Namba 10B: Stand United FC 2-1 Rhino Rangers FC

Klabu za Stand United na Rhino Rangers zimepewa onyo kwa kosa la kuwakilishwa na maafisa pungufu kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Mbao na Rhino ziliwakilishwa na maafisa wanne (4) kila moja badala ya watano (5) walioainishwa kikanuni.

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:2(2.2) na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

Mechi Namba 11B: TMA FC 2-0 Alliance FC

Klabu ya Alliance imepewa onyo kwa kosa la kutoingia kwenye chumba cha kuvalia katika mchezo tajwa hapo juu kwa kile walichoeleza kuwa walisahau ufunguo wa mlango wa chumba hicho ambao walikabidhiwa kwenye kikao cha maandalizi ya mchezo (MCM).

Adhabu hii ni kwa uzingativu wa Kanuni ya 18:20 na 18:60 ya First League kuhusu Taratibu za Mchezo.

 

 

RUVU SHOOTING, PRISONS HAKUNA MBABE

TIMU ya Ruvu Shooting imeshindwa kupata ushindi katika mchezo wa sita mfululizo baada ya kulazimishwa sare ya bao moja na Tanzania Prisons katika mchezo uliochezwa uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Tanzania Prisons ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Samson Mbangula dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza lililodumu kwa dakika nane pekee kabla ya Ruvu kusawazisha kwa mkwaju wa penati dakika ya 58 kupitia kwa Abalkassim Suleiman.

Ruvu Shooting watajilaumu kwa kushindwa kutumia nafasi walizopata ikiwemo mkwaju wa penati aliokosa Abalkassim Suleiman dakika chache kabla ya mpira kumalizika.

Akizungumza baada ya mchezo kocha wa Ruvu Shooting Charles Mkwasa amesema kuwa timu yake ilistahili kupata alama tatu katika mchezo wa leo hivyo matokeo ya sare kwao ni sawa na kupoteza.

Naye kocha wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo ameonesha kufurahishwa na matokeo waliyopata na kukiri kwamba Ligi Kuu ya NBC msimu huu ni ngumu hivyo kupata alama moja ugenini si jambo dogo kwao.

“Ni faraja kwetu kupata alama moja ugenini kwani ligi ya msimu huu ni ngumu sana hivyo tutafanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata ushindi katika michezo yote ya nyumbani,” alisema Odhiambo.

Ligi Kuu NBC itaendelea tena Novemba 9 kwa michezo miwili, Azam FC watakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji katika uwanja wa Azam Complex huku Singida Big Stars ikiwakaribisha Simba SC katika uwanja wa CCM Liti mjini Singida.

 

HAPATOSHI KWA MKAPA LEO

Dar es Saalam na viunga vyake itasimama kwa dakika 90 kupisha mchezo wa kwanza wa ‘derby’ ndani ya msimu huu wa 2022/2023 ukizikutanisha Yanga SC na Azam FC katika uwanja wa Benjamin Mkapa leo Septemba 6, 2022 saa 1:00 usiku.

Mara ya mwisho  timu hizi zilikutana Aprili 6, 2022 katika uwanja wa Azam Complex Chamazi na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, mabao ya Yanga yalifungwa na Djuma Shabani na Fiston Mayele huku lile la Azam likifungwa na Rodgers Kola.

Ni wachezaji wanne tu kwa kila timu ambao walishiriki katika mchezo wa mwisho timu hizi zilipokutana lakini hivi sasa hawapo na timu hizo, kwa upande wa Yanga wachezaji hao ni Deus Kaseke, Saido Ntibanzokiza, Balama Mapinduzi na Yassin Mustafa huku kwa upande wa Azam wakiwa ni Mudathir Yahya, Charles Zulu, Mathias Kigonya na Never Tigere.

Azam ndio timu ya mwisho kuifunga Yanga kwenye Ligi Kuu kwa bao 1-0, bao lake Prince Dube walipofanya hivyo kwenye msimu wa 2020/2021, baada ya hapo Yanga wamecheza michezo 39 kwenye Ligi Kuu bila kupoteza.

Je ni Yanga kuendeleza rekodi ya kutokufungwa   ama Azam kutibua rekodi hiyo?.

MZUNGUKO WA PILI LIGI KUU YA NBC

Ligi Kuu ya NBC inaendelea hii leo kwa mchezo mmoja kuchezwa baina ya Ihefu SC na Namungo FC katika uwanja wa Uhuru kuanzia saa 10:00 alasiri.

Ihefu wanatumia uwanja wa Uhuru kama uwanja wao wa nyumbani baada ya uwanja wao wa Highland Estates kufungiwa kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Wakiongea na waandishi wa habari kocha wa makipa na nahodha wa kikosi cha Namungo wamesema wapo tayari Kwenda kuwakabili Ihefu SC kwa kuwa wamejiandaa vya kutosha.

“Mchezo wa mwanzo ulikuwa mgumu lakini kwavile tushajua Ligi iko vipi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunaondoka na alama tatu,” alisema Faruk Ramadhani Kocha wa makipa wa Namungo.

Wakati huo huo nahodha wa timu hiyo Reliants Lusajo alisema malengo waliyoyapanga msimu uliopita hayakufanikiwa lakini msimu huu wanaamini watafanya vizuri na kuweza kushika nafasi nne za juu.

Kocha na nahodha wa Ihefu SC walishindwa kutokea katika mkutano huo kutokana na kupata changamoto za usafiri wakiwa safarini kuja Dar es saalam.

Raundi ya pili itaendelea tena kesho Agosti 20,2022 kwa michezo mitatu, michezo miwili  ya mapema itazikutanisha Coastal Union na Yanga SC katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakati Dodoma Jiji wakiwakabili Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Liti mkoani Singida kuanzia saa 10:00 alasiri.

Mchezo wa mwisho kesho utachezwa saa 1:00 usiku kati ya Simba SC na Kagera Sugar katika uwanja wa Benjamin Mkapa.A

KIVUMBI CHA LIGI KUU YA NBC KUANZA LEO

Pazia la Ligi kuu ya NBC msimu wa 2022/2023 linafunguliwa rasmi  hii leo Agosti 15, 2022 kwa timu nne za Ihefu SC, Ruvu Shooting FC, Namungo FC na Mtibwa Sugar FC  kushuka katika viwanja viwili kuzisaka alama tatu.

Mchezo wa kwanza wa ufunguzi utazikutanisha Ihefu  dhidi ya Ruvu Shooting majira ya saa 10:00 alasiri katika dimba la Highland Estate, Mbarali  Mkoani Mbeya wakati mchezo wa pili utazikutanisha  Namungo dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Timu ya Namungo  inatumia uwanja wa Benjamin Mkapa kama uwanja wake wa nyumbani baada ya uwanja wao wa Majaliwa, Lindi kuwa  katika maboresho.

Msimu huu wa 2022/2023 unashirikisha jumla ya timu 16 ambapo kila timu itacheza jumla ya michezo 30 kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na  kufanya jumla ya  michezo 240 sawa na michezo 120 nyumbani na 120 ugenini kwa timu zote.

KLABU LIGI KUU ZINAVYOVUNA KUTOKA SEMINA YA UEFA

SEMINA ya Maendeleo ya Ligi inayoendeshwa na UEFA chini ya mradi wao wa UEFA Assist imeingia siku ya nne leo kwenye Hotel ya Golden Tulip iliyopo Dar es Salaam.

Leo washiriki wa semina hiyo inayotarajiwa kukamilika Januari 15, 2022, wamepata nafasi ya kujifunza masuala mbalimbali zikiwemo mbinu za kuziongezea kipato klabu zao.

Mkufunzi wa UEFA Assist, Kenneth Macleod akitoa somo la namna ya kuongeza kipato kwa klabu.

Semina hiyo inashirikisha viongozi na maafisa wa TFF na Bodi ya Ligi, viongozi na maafisa wa Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi.

KLABU, TFF, TPLB KUNUFAIKA NA MAFUNZO YA UEFA ASSIST

Tanzania imepata bahati ya kufikiwa na Programu ya UEFA ya Maendeleo ya Mpira wa Miguu (UEFA Assist) ambapo imeandaliwa semina maalum yenye lengo la kuboresha Ligi za Tanzania na Uendeshaji wa Mashindano nchini.

Programu hiyo ilianza Novemba 2021 kwa zoezi la kukusanya maoni ya wadau mbalimbali wakiwemo makocha, wachezaji, Wanahabari, viongozi wa Shirikisho na Bodi ya Ligi, viongozi wa klabu, wadhamini na washabiki.

Hatua ya pili ya Programu hiyo ni semina ambayo itaendeshwa na maafisa wa UEFA Assist kwenye hoteli ya Golden Tulip mkoani Dar es salaam kuanzia Januari 10 hadi 15, 2022.

Washiriki wa semina hiyo ni viongozi na maafisa wa TFF na Bodi ya Ligi, viongozi na maafisa wa klabu za Ligi Kuu (Mwenyekiti/Rais, Katibu/CEO, Mkurugenzi wa Ufundi na Afisa wa Fedha na Mipango).

Baada ya semina hiyo, Programu itaingia katika hatua ya tatu ambapo maafisa wa UEFA Assist watasimamia utekelezaji wa mapendekezo ya maboresho Ligi na Uendeshaji wa Mashindano nchini.