YANGA MGUU MMOJA FAINALI YA SHIRIKISHO

TIMU ya Yanga inayoshika nafasi ya kwanza katika Ligi Kuu ya NBC mpaka mzunguko wa 27 imeendeleza rekodi nzuri ya kushinda mechi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini mabao 2-0.

Mabao yaliyofungwa na mchezaji wa kimataifa wa Burkina Faso Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison wa Ghana yameiweka Yanga nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya fainali katika michuano hiyo.

Yanga imekuwa na rekodi ya kushinda michezo ya Kimataifa kwa asilimia 100 msimu huu ikishinda michezo yote iliyocheza uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hiyo itatupa karata yake ya pili dhidi ya Marumo nchini Afrika Kusini Mei 17 katika uwanja wa Peter Mokaba kwenye Mji wa Polokwane.

Katika mchezo huo wa marudiano Yanga inahitaji ushindi au sare ili kufuzu hatua ya Fainali kwa mara ya kwa katika historia ya timu hiyo kwenye ngazi ya kimataifa.

COSMOPOLITAN MABINGWA FIRST LEAGUE 2022/23

Timu ya Cosmopolitan ya Dar imefanikiwa kutwaa ubingwa wa First League msimu wa 2022/23 baada ya kuifunga Stand United mabao 3-1 kwenye mchezo wa kuhitimisha fainali hizo msimu huu.

Mchezo wa leo ulikua kama kisasi kwa Stand kwani timu hizo zilikutana katika hatua ya makundi kwenye mchezo ambao Stand iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kumaliza kinara katika kundi hilo mbele ya Cosmo.

Cosmo imemaliza mashindano hayo ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi (10) huku ikiwa timu iliyoruhusu mabao mengi pia ya kufungwa (sita).

Cosmo na Stand zimejihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Championship msimu wa 2023/24 baada ya kupanda daraja mbali na Stand kupeteza mchezo wa fainali.

Nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo ya First League hatua ya Nane Bora imeshikwa na Dar City baada ya kuifunga TMA ya Arusha kwa bao 1-0.

Dar City na TMA bado zina nafasi ya kupanda daraja msimu ujao zikilazimika kusubiri ligi ya Championship itakapofika tamati ili kufahamu timu watakazocheza nazo kuwania nafasi ya kushiriki ligi hiyo msimu ujao.

TAKWIMU: FAINALI YA KISASI NANE BORA

FAINALI ya First League hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuchezwa Mei 3, kwenye uwanja wa Azam, Dar es Salaam kati ya Stand United ya Shinyanga na Cosmopolitan ya Dar.

Timu hizi zilikutana hatua ya makundi katika mchezo ambao Stand ilishinda kwa bao moja lililofungwa na Tungu Robert dakika ya 70 kwa mkwaju wa penati.

Timu ya Stand mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote ikiwa imecheza michezo minne katika hatua ya nane bora ikishinda miwili na kutoka sare miwili.

Huku timu ya Cosmopolitan ikicheza michezo minne pia ikishinda miwili, kutoka sare mmoja na kufungwa mchezo mmoja pekee dhidi ya wapinzani wao wa fainali Stand.

Stand imefanikiwa kufunga mabao matano na kuruhusu mabao mawili ya kufungwa huku Cosmo ikifunga mabao saba na kuruhusu mabao matano ya kufungwa.

Fainali hiyo itatanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu saa 9:00 alasiri kati ya Dar City iliyofungwa na Cosmopolitan na TMA FC iliyopoteza mchezo wake wa kwanza wa First League hatua ya nane bora dhidi ya Stand siku ya Mei Mosi.

STAND, COSMO ZATINGA CHAMPIONSHIP

NUSU fainali ya First League hatua ya Nane Bora imetamatika Mei Mosi kwa michezo miwili iliyoshuhudia Stand United ya Shinyanga na Cosmopolitan ya Dar es Salaam zikifanikiwa kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Championship msimu wa 2023/24.

Stand United maarufu kama ‘Chama la Wana’ imefanikiwa kushinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya TMA Stars ya Arusha kwa mabao 2-1 katika mchezo uliokwenda hadi dakika 120 baada ya timu hizo kutoshana nguvu kwa bao 1-1 ndani ya dakika 90.

TMA ilikua ya kwanza kupata bao kupitia kwa David Rweyendera dakika ya 61 kabla ya Stand kusawazisha dakika ya 85 kupitia kwa Kimu Juma na bao la ushindi kufungwa na Maulid Fadhili zikiwa zimesalia dakika nne mchezo huo kwenda hatua ya mikwaju ya penati.

Nayo Cosmopolitan imefanikiwa kupanda daraja la Championship baada ya kuwafunga majirani zao wa Mkoa wa Dar timu ya Dar City mabao 2-1 ndani ya dakika 90 za mchezo.

Cosmopolitan ilikua ya kwanza kupata bao mapema dakika ya 10 kupitia kwa Adili Buha lililodumu kwa dakika nane pekee kabla ya Mansoor Yusuph kuisawazishia Dar City huku bao la ushindi likifungwa dakika ya 74 na Dominick Benjamin.

Ligi hiyo itamalizika Mei 3 kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya TMA na Dar City saa 9:00 alasiri kabla ya kushuhudia fainali itakayozikutanisha Stand United dhidi ya Cosmopolitan saa 1:00 usiku.

HAWA HAPA MIAMBA WA NUSU FAINALI NANE BORA

TIMU za Dar City na TMA Stars zimeungana na Cosmopolitan na Stand United katika nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora msimu wa 2022/23.

Dar City ilitoka suluhu dhidi ya African Lyon kwenye mchezo uliopigwa mapema saa 10:00 alasiri na kufikisha alama tano zilizowafanya kumaliza vinara wa kundi B kwa mabao mengi ya kufunga (mawili).

TMA FC ambayo mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote wa First League imemaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na alama tano sawa na Dar City ikizidiwa tofauti ya mabao ya kufunga baada ya kufanikiwa kupata bao moja kwenye mchezo dhidi ya African Lyon.

Baada ya matokeo hayo timu ya Dar City itacheza dhidi ya Cosmopolitan iliyomaliza nafasi ya pili katika kundi A huku TMA ikicheza dhidi ya Stand United iliyomaliza kinara wa kundi A.

Michezo hiyo ya nusu fainali inatarajiwa kupigwa Mei Mosi ambapo Stand United itaikaribisha TMA katika mchezo wa mapema saa 9:00 alasiri huku Dar City ikicheza na Cosmopolitan saa 1:00 usiku.

COSMOPOLITAN YAUNGANA NA STAND NUSU FAINALI

TIMU ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam imeungana na Stand United ya Shinyanga katika nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na timu ya Alliance ya Mwanza.

Licha ya Alliance kutoka nyuma na kusawazisha mabao mawili kupitia kwa Joseph Naftal haikutosha kuwasaidia kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

Cosmopolitan imefanikiwa kusonga mbele kwa tofauti ya bao moja dhidi ya Lipuli baada ya timu zote kufanikiwa kukusanya alama nne zikishinda mechi moja na kutoa sare moja huku mabao yake ya mchezo wa leo yakifungwa na Isaac Steven na Hamza Nganga.

Lipuli imefikisha alama nne baada ya kupata ushindi wa bao moja lililofungwa na Bakari Ramadhan dhidi ya Stand United iliyokwisha kufuzu nusu fainali katika mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 29 kwa michezo ya kundi B itakayokutanisha timu za Dar City na African Lyon zote za Dar es Salaam saa 10:00 alasiri na saa 1:00 usiku Rhino Rangers ya Tabora itawakaribisha TMA FC ya Arusha.

DAR CITY MAMBO SAFI, TMA IKIENDELEA KUTAMBA

TIMU ya Dar City kutoka Mkoani Dar es Salaam imefanikiwa kushinda mchezo wa kwanza katika mashindano ya First League hatua ya Nane Bora dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 2-1.

Dar City iliyopata suluhu mchezo wa kwanza dhidi ya TMA FC ya Arusha imekwea mpaka nafasi ya kwanza katika msimamo wa kundi B baada ya kufikisha alama nne huku mabao yake katika mchezo wa leo yakifungwa na Nassoro Kondo na Said Dunia huku bao pekee la Rhino likifungwa na Ramadhan Athuman.

Rhino Rangers italazimika kupata ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya TMA Aprili 29 ili kujihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora msimu huu kama ilivyofanya msimu uliopita kwenye mashindano yaliyofanyika mkoani Mwanza.

TMA ya Arusha imeendeleza rekodi yake ya kutokupoteza mchezo wowote wa First League msimu huu baada ya kupata ushindi wa bao moja dhidi ya African Lyon ya Dar.

Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Mabingwa Mkoa imekuwa na rekodi nzuri ikiwa timu iliyofungwa mabao machache mpaka sasa msimu huu (9).

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 28 kwa michezo miwili, Lipuli ya Iringa itakuwa mwenyeji wa Stand United ya Shinyanga saa 10:00 alasiri na Alliance ya Mwanza itacheza saa 1:00 usiku na Cosmopolitan ya Dar.

LIPULI, ALLIANCE HAKUNA MBABE, STAND YATINGA NUSU FAINALI

TIMU ya Lipuli ya Iringa ililazimika kusubiri hadi dakika ya 90 kupata bao la kusawazisha dhidi ya Alliance ya Mwanza na kufanikiwa kutoka na sare ya bao 1-1 katika mchezo wa First League hatua ya Nane Bora.

Alliance ilikua ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Benjamin Williams dakika ya 32 kabla ya Hemed Ally kuifungia Lipuli kwa mpira wa adhabu uliomshinda golikipa wa Alliance.

Matokeo hayo yanaweka hai matumaini ya timu hizo mbili kusonga mbele hatua ya nusu fainali ikiwa timu mojawapo itashinda mchezo wa mwisho na kuongoza kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga.

Stand United ya Tabora imefanikiwa kuwa timu ya kwanza kukata tiketi ya kucheza nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora baada ya kushinda mchezo wake wa pili dhidi ya Cosmopolitan ya Dar kwa bao moja.

Mkwaju wa penati uliopigwa na Tungu Robert dakika ya 72 ulitosha kuihakikishia Stand nafasi ya kucheza nusu fainali huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Lipuli ya Iringa utakaochezwa Aprili 28.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 27 kwa michezo miwili Kati ya Dar City ya Dar na Rhino Rangers ya Tabora saa 10:00 alasiri na TMA Stars ya Arusha itakua mwenyeji wa African Lyon ya Dar saa 1:00 usiku.

RHINO YAANZA KIBABE, TMA IKIENDELEZA REKODI

TIMU ya Rhino Rangers ya Tabora imeanza kibabe mashindano ya First League hatua ya Nane Bora kwa kutoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya African Lyon ya Dar kwenye mchezo wa kundi B uliopigwa saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa Azam.

Pamoja na African Lyon kutangulia kupata bao kipindi cha kwanza kupitia kwa Agiri Ngoda walishindwa kuhimili mashambulizi ya Rhino waliosawazisha kupitia kwa Ramadhan Abdallah na kupata bao la ushindi dakika ya mwisho lililofungwa na Masawe Masawe.

TMA Stars ya Arusha ilicheza na Dar City ya Dar es Salaam saa 1:00 usiku ikiwa ni mchezo wa pili wa kundi B uliomalizika kwa suluhu.

TMA imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo wowote wa First League msimu huu mpaka kufikia hatua ya Nane Bora huku ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache (9).

Rhino Rangers baada ya ushindi wa leo wanashika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi B wakifuatiwa na Dar City na TMA wenye alama moja kila timu baada ya sare ya leo huku nafasi ya mwisho ikishikwa na African Lyon.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 26 kwa michezo miwili ya kundi A itakayokutanisha timu za Lipuli dhidi ya Alliance mchezo wa saa 10:00 alasiri na Cosmopolitan itakua mwenyeji wa Stand United saa 1:00 usiku.

PRISONS YAMALIZA UBABE WA GEITA NYANKUMBU

TIMU ya Prisons ya Mbeya imemaliza ubabe wa Geita Gold ikicheza katika uwanja wake wa Nyankumbu kwa kuifunga Mabao 3-1.

Mchezo wa mwisho kwa Geita kufungwa uwanja wa Nyankumbu kabla ya kipigo cha leo ilikua dhidi ya timu ya Pamba kutoka Mwanza katika mchezo wa Ligi ya Championship msimu wa 2020/21.

Mabao ya Jeremiah Juma, Samson Mbangula na Edwin Balua yameifanya Prisons kuwa timu ya kwanza kuondoka na alama zote tatu dhidi ya Geita Gold kwenye uwanja wa Nyankumbu tangu timu hiyo ipande daraja.

Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa timu ya Prisons ikipanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 31.