Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza Ligi Kuu ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.
Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya sita mwaka 2023 hadi nafasi ya nne ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.
Kwa mujibu wa taarifa ya IFFHS kwa upande wa Afrika nchi zilizoko chini ya Shirikisho la Soka (CAF) Ligi Kuu ya Misri inayofahamika kama Nile Premier League ndio kinara kwa ubora Afrika.
Nafasi ya pili inashikiliwa na Botola Pro ambayo ni Ligi Kuu ya Morocco huku League 1 ya Algeria ikishika nafasi ya tatu kwa ubora mwaka 2024.
Kwa upande wa Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania imekwea hadi nafasi ya nne barani Afrika kutokana na ligi hiyo kuwa na usimamizi bora kuanzia Serikali, Shirikisho la Soka nchini (TFF), Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Klabu zinazoshiriki ligi hiyo, wadhamini mbalimbali wanavyounga mkono pamoja na mashabiki.