LIGI Kuu ya NBC inaendelea leo Februari 7, 2025 kwa michezo miwili kuchezwa kwenye mikoa ya Arusha na Singida kuanzia saa 10:00 Alasiri.
Mkoani Arusha Coastal Union itaikaribisha JKT Tanzania kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid huku ikiingia kwenye mchezo huu ikishika nafasi ya 11 ikikusanya alama 18 kwenye michezo 16 na JKT Tanzania ikishika nafasi ya nane baada ya kukusanya alama 19 wakiwa na tofauti ya alama moja (1) pekee kati yao.
Mkoani Singida, timu ya Singida Black Stars itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar ya mkoani Kagera kwenye uwanja wa CCM Liti huku mara ya mwisho timu hizi kukutana Agosti 24, 2024 mkoani Kagera, Singida Black Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 likifungwa na Mchezaji Anthony Tra Bi dakika ya 90+3 ya mchezo huo.
Michezo hii miwili inakamilisha michezo ya mzunguko wa 17 wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2024/2025 ambapo mpaka sasa timu ya Young Africans ikishika usukani na alama 45 huku Kengold ikiburuza mkia ikiwa na alama sita pekee.