Author: Honest Mwanitega

TAKWIMU: FAINALI YA KISASI NANE BORA

FAINALI ya First League hatua ya Nane Bora inatarajiwa kuchezwa Mei 3, kwenye uwanja wa Azam, Dar es Salaam kati ya Stand United ya Shinyanga na Cosmopolitan ya Dar.

Timu hizi zilikutana hatua ya makundi katika mchezo ambao Stand ilishinda kwa bao moja lililofungwa na Tungu Robert dakika ya 70 kwa mkwaju wa penati.

Timu ya Stand mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote ikiwa imecheza michezo minne katika hatua ya nane bora ikishinda miwili na kutoka sare miwili.

Huku timu ya Cosmopolitan ikicheza michezo minne pia ikishinda miwili, kutoka sare mmoja na kufungwa mchezo mmoja pekee dhidi ya wapinzani wao wa fainali Stand.

Stand imefanikiwa kufunga mabao matano na kuruhusu mabao mawili ya kufungwa huku Cosmo ikifunga mabao saba na kuruhusu mabao matano ya kufungwa.

Fainali hiyo itatanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu saa 9:00 alasiri kati ya Dar City iliyofungwa na Cosmopolitan na TMA FC iliyopoteza mchezo wake wa kwanza wa First League hatua ya nane bora dhidi ya Stand siku ya Mei Mosi.

STAND, COSMO ZATINGA CHAMPIONSHIP

NUSU fainali ya First League hatua ya Nane Bora imetamatika Mei Mosi kwa michezo miwili iliyoshuhudia Stand United ya Shinyanga na Cosmopolitan ya Dar es Salaam zikifanikiwa kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Championship msimu wa 2023/24.

Stand United maarufu kama ‘Chama la Wana’ imefanikiwa kushinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya TMA Stars ya Arusha kwa mabao 2-1 katika mchezo uliokwenda hadi dakika 120 baada ya timu hizo kutoshana nguvu kwa bao 1-1 ndani ya dakika 90.

TMA ilikua ya kwanza kupata bao kupitia kwa David Rweyendera dakika ya 61 kabla ya Stand kusawazisha dakika ya 85 kupitia kwa Kimu Juma na bao la ushindi kufungwa na Maulid Fadhili zikiwa zimesalia dakika nne mchezo huo kwenda hatua ya mikwaju ya penati.

Nayo Cosmopolitan imefanikiwa kupanda daraja la Championship baada ya kuwafunga majirani zao wa Mkoa wa Dar timu ya Dar City mabao 2-1 ndani ya dakika 90 za mchezo.

Cosmopolitan ilikua ya kwanza kupata bao mapema dakika ya 10 kupitia kwa Adili Buha lililodumu kwa dakika nane pekee kabla ya Mansoor Yusuph kuisawazishia Dar City huku bao la ushindi likifungwa dakika ya 74 na Dominick Benjamin.

Ligi hiyo itamalizika Mei 3 kwa mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya TMA na Dar City saa 9:00 alasiri kabla ya kushuhudia fainali itakayozikutanisha Stand United dhidi ya Cosmopolitan saa 1:00 usiku.

HAWA HAPA MIAMBA WA NUSU FAINALI NANE BORA

TIMU za Dar City na TMA Stars zimeungana na Cosmopolitan na Stand United katika nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora msimu wa 2022/23.

Dar City ilitoka suluhu dhidi ya African Lyon kwenye mchezo uliopigwa mapema saa 10:00 alasiri na kufikisha alama tano zilizowafanya kumaliza vinara wa kundi B kwa mabao mengi ya kufunga (mawili).

TMA FC ambayo mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote wa First League imemaliza nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na alama tano sawa na Dar City ikizidiwa tofauti ya mabao ya kufunga baada ya kufanikiwa kupata bao moja kwenye mchezo dhidi ya African Lyon.

Baada ya matokeo hayo timu ya Dar City itacheza dhidi ya Cosmopolitan iliyomaliza nafasi ya pili katika kundi A huku TMA ikicheza dhidi ya Stand United iliyomaliza kinara wa kundi A.

Michezo hiyo ya nusu fainali inatarajiwa kupigwa Mei Mosi ambapo Stand United itaikaribisha TMA katika mchezo wa mapema saa 9:00 alasiri huku Dar City ikicheza na Cosmopolitan saa 1:00 usiku.

COSMOPOLITAN YAUNGANA NA STAND NUSU FAINALI

TIMU ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam imeungana na Stand United ya Shinyanga katika nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na timu ya Alliance ya Mwanza.

Licha ya Alliance kutoka nyuma na kusawazisha mabao mawili kupitia kwa Joseph Naftal haikutosha kuwasaidia kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

Cosmopolitan imefanikiwa kusonga mbele kwa tofauti ya bao moja dhidi ya Lipuli baada ya timu zote kufanikiwa kukusanya alama nne zikishinda mechi moja na kutoa sare moja huku mabao yake ya mchezo wa leo yakifungwa na Isaac Steven na Hamza Nganga.

Lipuli imefikisha alama nne baada ya kupata ushindi wa bao moja lililofungwa na Bakari Ramadhan dhidi ya Stand United iliyokwisha kufuzu nusu fainali katika mchezo wa mapema saa 10:00 alasiri.

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 29 kwa michezo ya kundi B itakayokutanisha timu za Dar City na African Lyon zote za Dar es Salaam saa 10:00 alasiri na saa 1:00 usiku Rhino Rangers ya Tabora itawakaribisha TMA FC ya Arusha.

DAR CITY MAMBO SAFI, TMA IKIENDELEA KUTAMBA

TIMU ya Dar City kutoka Mkoani Dar es Salaam imefanikiwa kushinda mchezo wa kwanza katika mashindano ya First League hatua ya Nane Bora dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 2-1.

Dar City iliyopata suluhu mchezo wa kwanza dhidi ya TMA FC ya Arusha imekwea mpaka nafasi ya kwanza katika msimamo wa kundi B baada ya kufikisha alama nne huku mabao yake katika mchezo wa leo yakifungwa na Nassoro Kondo na Said Dunia huku bao pekee la Rhino likifungwa na Ramadhan Athuman.

Rhino Rangers italazimika kupata ushindi katika mchezo wa mwisho dhidi ya TMA Aprili 29 ili kujihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali ya First League hatua ya Nane Bora msimu huu kama ilivyofanya msimu uliopita kwenye mashindano yaliyofanyika mkoani Mwanza.

TMA ya Arusha imeendeleza rekodi yake ya kutokupoteza mchezo wowote wa First League msimu huu baada ya kupata ushindi wa bao moja dhidi ya African Lyon ya Dar.

Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Mabingwa Mkoa imekuwa na rekodi nzuri ikiwa timu iliyofungwa mabao machache mpaka sasa msimu huu (9).

Ligi hiyo itaendelea tena Aprili 28 kwa michezo miwili, Lipuli ya Iringa itakuwa mwenyeji wa Stand United ya Shinyanga saa 10:00 alasiri na Alliance ya Mwanza itacheza saa 1:00 usiku na Cosmopolitan ya Dar.