ATEBA AIZAMISHA KENGOLD LIGI KUU NBC

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana katika uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kwa timu ya Simba kuwakaribisha wachimba dhahabu wa mkoani Mbeya timu ya KenGold saa 10:00 alasiri.

Dakika ya 34 ya mchezo huo mshambuliaji wa Simba Leonel Ateba alifunga goli kwa mkwaju wa penati baada ya kiungo wao Awesu Awesu kufanyiwa madhambi na mchezaji wa KenGold.

Ilimchukua dakika 10 Ateba kuiongezea bao timu yake akipokea pasi kutoka kwa beki wa kushoto Valentin Nouma aliyepiga kona hivyo kuifanya timu yao kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu ya Simba kushambulia kwa kasi lango la mpinzani wao hata hivyo walishindwa kutikisa nyavu za mpinzani wao baada ya kudhibitiwa vyema na mabeki wa KenGold na mchezo kutamatika kwa Simba kushinda 2-0.

Simba imefanikiwa kupanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Azam wenye alama 33 baada ya kufikisha alama 31 wakiishusha timu ya Singida Black Stars yenye alama 30.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo mkoani Dar es Salaam kwa mchezo mmoja ambapo timu ya Yanga itaikaribisha timu ya Mashujaa kutoka mkoani Kigoma saa 10:00 alasiri.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *