TIMU ya Mtibwa Sugar inayoshikilia usukani wa Ligi ya Championship ya NBC imeendelea kuwa ‘Mwiba’ kwa timu za ligi hiyo kwa kushinda michezo mingi nyumbani na ugenini kuliko timu zote.
Mtibwa imeshinda michezo 11 nyumbani kwenye uwanja wa Manungu Complex, Morogoro huku ikishinda sita kwenye michezo yake ya ugenini na kuwa kinara wa ushindi nyumbani na ugenini.
Geita Gold inafuata ikiwa imeshinda michezo 10 kwenye uwanja wa Nyankumbu, Geita huku ikishinda minne ugenini sawa na timu za Mbeya Kwanza na Songea United.
Stand United ya Shinyanga na TMA FC ya Arusha zinashika nafasi ya tatu kwa kushinda michezo mingi kwenye uwanja wa nyumbani zikishinda michezo 9.