NBC CHAMPIONSHIP KUANZA KUTIMUA VUMBI LEO

LIGI ya NBC Championship inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo kwa michezo miwili kupigwa kwenye mikoa ya Kagera na Arusha.

Majira ya saa 10:00 alasiri Kagera Sugar iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya NBC inatarajiwa kucheza karata yake ya kwanza leo kwenye uwanja wa Kaitaba, Kagera dhidi ya Transit Camp ili kutafuta nafasi ya kurejea kwa mara nyingine ligi hiyo.

Timu hiyo ‘inayonolewa’ na mchezaji wa zamani wa Taifa Stars (Tanzania) Juma Kaseja imedhamiria kufanya vizuri msimu huu ikiwa imesajili wachezaji wenye uzoefu na waliocheza Ligi Kuu ya NBC wakiwemo Andrew Vicent (Chikupe), Joseph Mahundi, Fredy Tangalo na Hassan Mwaterema.

Kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha timu ya Mbuni itakuwa mwenyeji wa Mbeya kwanza ya Mtwara saa 10:00 alasiri.

Mbuni iliyomaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ya NBC ya Championship inatarajia kuivaa Mbeya Kwanza iliyomaliza nafasi ya saba ikishindwa kucheza hatua ya mtoano msimu uliopita kwa tofauti ya alama sita pekee.

Ligi ya NBC Championship inatarajiwa kupata bingwa mpya msimu huu baada ya bingwa mtetezi timu ya Mtibwa Sugar kupanda Ligi Kuu ya NBC na hivyo kushindwa kutetea ubingwa wake.

Chaneli ya Fifa Plus itaonyesha mchezo kati ya Mbuni na Mbeya Kwanza moja kwa moja na itaendelea kufanya hivyo kwenye michezo mingine ya Ligi ya Championship ya NBC msimu wa 2025/26.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *