LIGI Kuu ya NBC inatarajiwa kushuhudia mchezo kati ya Mbeya City na Prisons (Mbeya Derby) kwenye uwanja wa KMC Complex kwa mara ya kwanza ukipigwa mkoani Dar es Salaam huku timu zote asili yake ikiwa ni mkoani Mbeya.
Hii inatokea baada ya timu ya Mbeya City kuuchagua uwanja wa KMC kama uwanja wake wa nyumbani badala ya uwanja Sokoine uliofungiwa na kamati ya ukaguzi kupisha marekebisho.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa Disemba 25, 2022 na Tanzania Prisons kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huo ukimalizika kwa sare ya bao moja.
Mbeya City inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya NBC hadi sasa ikiwa na alama saba baada ya kushinda michezo miwili, sare mmoja na kupoteza mmoja inakutana na ‘Wajelajela’ Prisons walioshinda mchezo mmoja pekee na kupoteza miwili huku wakikamata nafasi ya 13 kwenye msimamo.
Mchezaji wa Mbeya City Soudy Dondola amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Prisons utakuwa mgumu lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kuwapa furaha mashabiki wa Mbeya City.
“Morali ni ya kutosha kuelekea mchezo wetu, tunatambua ni mchezo muhimu sana kwetu kupata ushindi ili tuwe na muendelezo mzuri wa msimu. Alisema Soudy.
Nae Dotto Shabani wa Tanzania Prisons amesema wamejipanga vizuri kuendeleza ubabe dhidi ya Mbeya City ingawa haiwezi kuwa kazi nyepesi wao kufanya hivyo.
” Kiu yetu kubwa ni kuifunga Mbeya City na kuendeleza ubabe dhidi yao ingawa mchezo lazima utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu kuanza msimu vizuri na wakiwa vinara hadi sasa.” alisema Dotto.
Mchezo huo utaanza saa 10:00 alasiri na kuonyeshwa mbashara kwenye chaneli ya Azam Sports huku matangazo ya redio yakirushwa moja kwa moja na kituo cha TBC.