TIMU ya Coastal Union imeonyesha ubabe ugenini katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-1.
Mchezo ulianza kwa kasi Coastal Union wakipata bao la mapema zaidi kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu lililofungwa sekunde ya 58 kupitia kwa Bakari Msimu na dakika tatu kabla ya mchezo kwenda mapumziko Shiza Kichuya aliongeza jingine kwa kichwa akipokea pasi safi kutoka kwa Bakari Msimu.
Tanzania Prisons haikukata tamaa na kuendelea kushambulia jitihada zilizozaa matunda dakika ya 45+2 kupitia kwa George Mpole aliyewafungia bao lililowapa matumaini kabla ya mapumziko.
Dakika ya 51 Bakari Msimu aliongeza bao lake la pili katika mchezo huo na kuifanya Coatal kuongoza 3-1 kabla ya Cleophace Mkandala kuhitimisha karamu ya mabao kwa kufunga dakika ya 90+5 na kuhitimisha ushindi mnono wa mabao 4-1.
Mchezo mwingine uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza na Pamba Jiji kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo.
Bao pekee la mchezo huo lilifungwa dakika ya 55 kupitia kwa Mathew Tegisi lililodumu hadi mwisho wa dakika 90 na kuwapa Pamba Jiji alama tatu muhimu.