Ligi Kuu ya NBC inaendelea kutimua vumbi leo, Machi 11, 2026, ambapo jumla ya michezo mitatu itapigwa katika mikoa ya Arusha, Singida na Dodoma, huku timu mbalimbali zikiingia uwanjani kusaka alama muhimu katika mbio za msimamo wa ligi.
Mchezo wa mapema utapigwa katika Uwanja wa Black Rhino, Karatu mkoani Arusha, ambapo TRA United itakuwa mwenyeji wa Namungo FC. TRA United inaingia kwenye pambano hilo ikiwa na alama 16 baada ya kucheza michezo 13 ya ligi hadi sasa.
Kwa upande wa Namungo FC, inayofundishwa na Kocha Juma Mgunda, inaingia katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, ikiwa imekusanya alama 21 baada ya kucheza michezo 16.
Mkoani Singida,mashabiki watashuhudia pambano jingine la kusisimua litakalowakutanisha Singida Black Stars dhidi ya Simba SC katika Uwanja wa Airtel, kuanzia majira ya saa 10:15 jioni.
Singida Black Stars inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi yake iliyopita kwa mabao 3-0 dhidi ya Young Africans. Kwa upande wake Simba SC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Young Africans katika mchezo wake wa mwisho wa ligi.
Mchezo wa mwisho wa leo utapigwa katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, ambapo Dodoma Jiji itamenyana na Azam FC kuanzia saa 1:15 usiku.
Mara ya mwisho timu hizi mbili kukutana kwenye Ligi Kuu ya NBC ilikuwa Mei 13, 2025 katika Uwanja wa Azam Complex, ambapo Azam FC iliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0.
Mashabiki wa soka wanaweza kufuatilia michezo yote ya leo mubashara kupitia king’amuzi cha Azam TV kwenye chaneli ya Azam Sports 1 HD, au kusikiliza matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC FM.