Author: Yahaya Abushehe

Wachezaji wa Biashara United wakishangilia bao pekee walilofunga dhidi ya African Sports kwenye mchezo uliopigwa uwanja wa Karume, Mara.

BIASHARA YAFUFUA MATUMAINI MZUNGUKO UKIKAMILIKA NBC CHAMPIONSHIP.

MZUNGUKO wa 23 wa Ligi ya Championship ya NBC umehitimishwa jana kwa mchezo mmoja kuchezwa katika uwanja wa Karume Mkoani Mara na kushuhudia Biashara United ikiibuka na Ushindi wa Bao 1-0 dhidi ya African Sports.

Licha ya Ushindi huo Biashara United inaendelea kusalia nafasi ya mwisho kwenye msimamo ikifikisha alama saba baada ya michezo 23.

Ikumbukwe Biashara United ilipokwa alama 15 baada ya kushindwa kutokea kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City.

Mtibwa Sugar inaendelea kusalia kileleni licha ya kupoteza kwenye mchezo wake dhidi ya Stand United ikiwa na alama 54 baada ya michezo 23 ikifuatiwa na Mbeya City na Stand United kwa pamoja zikiwa na alama 49 zikipishana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

STAND UNITED

NI VITA YA ‘TOP FOUR’ NBC CHAMPIONSHIP LEO.

MICHEZO mitatu ya Ligi ya Championship ya NBC inapigwa leo Machi 17 ambapo mikoa ya Geita, Mbeya na Shinyanga itakuwa wenyeji wa michezo hiyo.

Michezo ya Leo inazikutanisha baadhi ya timu zinazopambana kujiweka vizuri kwenye nafasi nne za juu za msimamo wa Ligi ya Championship ya NBC.

Stand United iliyo nafasi ya tatu na alama 46 itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar iliyo nafasi ya kwanza na alama 54 kwenye uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Mkoani Geita, Geita Gold inayoshika nafasi ya nne ikiwa na alama 45 itakuwa mwenyeji wa Mbeya Kwanza iliyo nafasi ya sita na alama 39 kwenye uwanja wa Nyankumbu.

Mchezo wa Mwisho leo utazikutanisha Mbeya City inayoshika nafasi ya pili dhidi ya Kiluvya iliyo nafasi ya 12 kwenye uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya huku michezo yote ya Leo itaanza kuanzia majira ya saa 10:00 za alasiri.

NBC CHAMPIONSHIP ‘BOLI’ LINACHEZWA.

TAYARI michezo 176 kati ya 240 ya Ligi ya Championship ya NBC imeshachezwa huku ushindani mkubwa ukionekana baina ya timu zinazoshiriki ligi hiyo ambayo Mtibwa Sugar ipo kileleni kwasasa ikiwa na alama zake 54 baada ya michezo 22 ya Ligi hiyo.

Kwa upande wa nafasi nne za juu ushindani ni mkubwa huku kila timu zikitafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya NBC moja kwa moja ambapo nafasi hizo nne za juu zinashikiliwa na Mtibwa akiwa nafasi ya kwanza na alama 54, Mbeya City ikiwa nafasi ya pili ikiwa na alama 46 sawa na Stand United iliyo nafasi ya tatu wakitofautiana kwenye mabao ya kufunga na kufungwa na nafasi ya nne ikishikiliwa na Geita Gold yenye alama 45.

Cosmopolitan, African Sports, Transit Camp na Biashara United zinaendelea kupambana kwenye nafasi nne za chini kujinasua kutokushuka daraja kwa msimu huu, Biashara United inaburuza mkia kwenye Ligi hiyo ikiwa na alama nne pekee, Transit Camp ipo nafasi ya 15 ikiwa na alama 11, African Sports inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 14 wakati Cosmopolitan ikiwa na alama 15 kwenye nafasi ya 13.

Timu mbili za juu kwenye msimamo zinapanda moja kwa moja kwenye Ligi Kuu ya NBC huku mbili za mwisho zikishuka moja kwa moja na kushiriki First League.

ARAJIGA

ARAJIGA PILATO WA ‘DERBY’ YA KARIAKOO.

BODI ya Ligi Kuu Tanzania leo Februari 5, imetangaza orodha ya maofisa watakaosimamia mchezo wa ‘DERBY’ ya Kariakoo wakiwemo waamuzi wa mchezo huo, Ahmed Arajiga kutoka Manyara aliyeteuliwa kuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Mohamed Mkono kutoka Tanga na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Amina Kyando kutoka Morogoro.

Maofisa wengine walioteuliwa kusimamia mchezo huo ni Pamoja na Salim Singano Kamisaa wa Mchezo, Soud Abdi Mtathmini wa Waamuzi, Baraka Kizuguto Mratibu wa Mchezo, Jonas Kiwia Mratibu wa Mchezo Msaidizi, Karim Boimanda Afisa Habari, Fatma Abdallah Afisa Protokali, Jerry Temu Afisa Masoko, Manfred Limbanga Daktari wa mchezo, ASP Hashim Abdallah Afisa Usalama na Ramadhan Misiru Msimamizi wa Kituo.

Ni siku tatu pekee zimesalia kwenda kushuhudia mchezo huo mkubwa zaidi kwenye Ligi namba nne (4) kwa ubora barani Afrika.

DIARRA, CAMARA

HUKU DIARRA KULE CAMARA MILANGO IPO SALAMA.

Zimesalia siku nne kuelekea kwenye kwenye ‘DERBY’ ya Kariakoo ambapo Young Africans itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 8, 2025 kuanzia saa 1:15 usiku.

Young Africans na Simba zinaingia kwenye mchezo huu zikiwa ndio timu zilizoruhusu mabao machache zaidi ya kufungwa, Young Africans ikiruhusu tisa (9) huku Simba ikiruhusu mabao nane (8) pekee.

Moussa Camara wa Simba anaongoza kwa kuwa na hati safi (Cleansheets) akiwa nazo 15 kwenye michezo 20 aliyocheza akitumia jumla ya dakika 1800 huku Djigui Diarra wa Young Africans akifuatia akiwa nazo 11 kwenye michezo 15 aliyoitumikia Young Africans msimu huu akitumia jumla ya dakika 1451.

Ubora wa walinda milango hawa umezifanya timu za Young Africans na Simba kuwa na wastani mdogo wa mabao ya kufungwa hivyo kuufanya mchezo huu wa ‘Derby’ ya kariakoo kuwa na mvuto wa aina yake.