BEKI wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro amechaguliwa kuwa mchezaji Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku Steve Barker wa Simba akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Imoro alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo kwa mwezi huo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu katika michezo mitano ambayo Singida ilicheza na kuisaidia timu yake kupanda kutoka nafasi ya 10 hadi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Beki huyo aliwashinda Anicet Oura wa Simba na Lamine Jarjou wa Singida Black Stars alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa upande wa Barker aliyeingia fainali na Pedro Goncalves wa Yanga na David Ouma wa Singida Black Stars, aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili na kupanda kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Airtel mkoani Singida, Omar Malule, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Machi kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Katika hatua nyingine Omari Mponda wa Mbuni amechaguliwa Mchezaji Bora wa Mwezi Machi wa Ligi ya NBC Championship 2025/26, huku Zuberi Katwila wa Geita Gold, akichaguliwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Mponda aliyeingia fainali na Yusuf Mhilu na Maulid Shaaban wote wa Geita Gold alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili kwa dakika 155 za michezo miwili aliyotumika mwezi huo.

Kwa upande wa Katwila aliyeingia fainali na Leonard Budeba wa Mbuni na Twaha Beimbaya wa B19, aliiwezesha timu yake kushinda michezo yote miwili iliyocheza na kupanda kutoka nafasi ya pili hadi ya kwanza kwenye msimamo wa ligi.
Pia Kamati ya Tuzo imeteua magoli matatu bora ambayo yatapigiwa kura na mashabiki wa mpira wa miguu nchini, ili kupata Tuzo ya Goli Bora la Mashabiki kwa mwezi Machi.
Magoli hayo ni Prince Dube (Singida v Yanga dakika ya 38), Joseph
Akandwanaho (TRA v Namungo dakika 90+1) na Ibrahim Imoro (Mbeya City v
Singida Black Stars dakika ya 86).