MSIMU wa Ligi Kuu ya NBC unaendelea huku ushindani wa mabao ya nje ya boksi ukishika kasi na wachezaji wakionyesha uwezo mkubwa wa kupiga mashuti ya mbali na kufunga mabao ya kuvutia.
Kinara wa orodha hiyo ni Ismail Mhesa kutoka Mtibwa Sugar akiwa amefunga mabao matatu nje ya boksi na kuonyesha ubora mkubwa wa kupiga mbali na kuwa tegemeo kwa timu yake akifunga mabao hayo walipokutana na timu za Prisons, Young Africans na TRA.
Sambamba naye ni Iddi Selemani wa Azam ambaye pia ana mabao 3 huku akiendelea kuwa na mchango mkubwa kwa timu yake ya Azam akitumia ubunifu na uwezo wa kufunga akiwa nje ya eneo la hatari na akifanya hivyo mara mbili alipokutana na KMC huku bao moja akiwafunga TRA.
Nafasi ya tatu inashikiliwa na Ibrahim Imoro anayekipiga Singida Black Stars akiwa na mabao matatu ambayo aliyapata walipokutana dhidi ya Prison na Mbeya City huku akinyesha uthabiti mkubwa katika mashuti ya mbali na kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji ya timu yake ingawa yeye ni mlinzi.
Wakati huo huo Libase Gueye wa Simba SC ana mabao mawili ya nje boksi akionyesha ubora wake wa kushambulia kwa kutumia nafasi chache anazopata na mabao hayo akiyapata dhidi ya Mashujaa na KMC.
Orodha hiyo inakamilishwa na Kelvin Nashon kutoka KMC mwenye mabao mawili aliyofunga walipokutana na Mbeya City na Singida black star na kumfanya kiungo huyo raia wa Tanzania kuwa tishio kwa timu pinzani.
Kwa ujumla wachezaji wa Ligi Kuu wanazidi kuboresha uwezo wa kufunga mabao ya mbali jambo linaloongeza burudani na ushindani mkubwa ndani ya Ligi.