DODOMA YAISIMAMISHA YOUNG AFRICANS, COASTAL IKIILIZA MBEYA CITY.

TIMU ya Dodoma Jiji imemaliza utemi wa timu ya Young Africans wa kucheza michezo zaidi ya 40 bila kufungwa katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kuifunga 3-2 kwenye uwanja wa Airtel Stadium, Singida huku timu ya Mbeya City ikikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa timu ya Coastal Union.

Dakika mbili zilimtosha kiungo wa Young Africans,Allan Okello kufungua ukurasa wa mabao kwa kuitanguliza Young Africans lililodumu kwa dakika 27 kabla ya beki wa wababe hao wa Kariakoo Bakari Mwamunyeto kujifunga na kufanya ubao usome 1-1 kabla ya Okello kurejea tena nyavuni dakika ya 41 na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko ‘Wananchi’ wakiongoza 1-2.

Kipindi cha pili Dodoma Jiji walirejea kwa kasi kubwa ikiwa azma yao kubwa n kuhakikisha alama zinabaki nyumbani na dakika ya 89 Mwana Kibuta alifunga bao la pili kwa Dodoma kabla ya Waziri Junior kupeleka kilio ‘Jangwani’ kwa bao la tatu ndani ya dakika za nyongeza hivyo mchezo kuisha kwa matokeo ya 3-2.

Young Africans imesalia kileleni ikiwa na alama 54 huku Dodoma Jiji ikipanda nafasi ya saba na alama 32.

Mchezo mwingine wa mapema ulichezwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambapo Mbeya City iliikaribisha timu ya Coastal Union ya Tanga mchezo na kushuhudia ‘Wagosi wa kaya’ wakiondoka na alama zote tatu baada ya ushindi wa mabao 2-0.

Ilimchuka dakika 35 mshambuliaji wa Coastal Maabad Maabad kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati hivyo kwenda mapumziko wakiongoza na kujitengenezea nafasi nzuri kwao kujinasua kutoka nafasi za chini ya msimamo.

Kipindi cha pili dakika ya 74 Saad Mwanza aliiongezea bao la pili Coastal hivyo mchezo kumalizika wakiwa kifua mbele kwa mabao mawili na alama zote tatu.

Matokeo hayo yanaiweka Coastal nafasi ya 11 na alama 25 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya 13 na alama 21 ikiwa ni nafasi ya timu zinazocheza mtoano wa kusalia Ligi Kuu ya NBC.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *