YOUNG AFRICANS,AZAM ZATAKATA NYUMBANI LIGI KUU YA NBC.

Ligi Kuu ya NBC imeendelea kushika kasi huku vigogo wakionyesha makali yao ambapo timu ya Young Africans na Azam zikifanikiwa kupata alama tatu muhimu kwenye viwanja vyao vya nyumbani.

Katika Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam mchezo wa kwanza uliwakutanisha mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Namungo na kushuhudia ‘Wananchi’ wakipata ushindi wa 3-1.

Yanga ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 26 kupitia Duke Abuya baada ya shambulizi lililovunja ukuta wa Namungo na hata hivyo ‘Wauaji wa kusini’ walirejea mchezoni dakika ya 40 kupitia Hassan Kabunda na kufanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kiungo Allan Okello wa Yanga alifunga mabao mawili dakika ya 52 na 84 na kuihakikishia timu yake ushindi huo.

Okello pia alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, akiendelea kuthibitisha ubora wake tangu aliposajiliwa dirisha la mwezi Januari ambapo sasa amefikisha mabao 11 kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu huku ushindi huo kwa Yanga ukiifanya timu hiyo kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.

Katika mchezo mwingine uliochezwa saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Chamazi wenyeji Azam waliibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya timu inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo.

Kiungo nyota Feisal Salum alianza kuifungia Azam mapema dakika ya 2 kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 16 na kuendelea kuonyesha kiwango bora msimu huu akiwa ndiye kinara wa mabao hadi sasa akifunga mabao 14 hadi sasa .

Yoro Diaby akahitimisha karamu ya mabao dakika ya 34 na kuhakikisha KMC inaondoka bila alama yoyote wala bao huku kiungo Feisal akiibuka mchezaji bora wa mchezo huo.

Matokeo hayo yanaendelea kuongeza presha katika mbio za nafasi za juu huku kila mchezo ukiwa na uzito mkubwa kuelekea mwisho wa msimu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *