MBEYA CITY, YOUNG AFRICANS, SINGIDA ZATAMBA LIGI KUU YA NBC.

 

LIGI Kuu ya NBC iliendelea jana kwa michezo mitatu iliyokuwa na ushindani mkubwa, huku vinara Young Africans wakiendelea kuimarisha nafasi yao kileleni mwa msimamo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Kiungo Mudathir Yahya aliwatanguliza ‘wananchi’ mbele dakika ya 29 kabla ya beki Bakari Mwamnyeto kufunga bao la pili dakika ya 90+1 na kuhakikisha mabingwa watetezi wanaondoka na alama tatu muhimu.

Ushindi huo umeifanya Young Africans kuendelea kushikilia nafasi ya kwanza kwa alama 63.

Katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya City ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwa bao pekee la mchezo lilifungwa na Adili Buha dakika ya 35 kwa mkwaju wa penati huku matokeo hayo yakiipa Mbeya City alama muhimu katika harakati za kujinasua kutoka maeneo ya hatari.

Mchezo mwingine uliopigwa jijini Dar es Salaam uliwakutanisha JKT Tanzania na Singida Black Stars, ambapo wageni waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Horso Muaku aliifungia Singida Black Stars bao la kwanza dakika ya 23 kabla ya Emmanuel Keyekeh kuongeza la pili dakika ya 75 na JKT Tanzania wakipata bao la kufutia machozi kupitia Valentino Mashaka dakika ya 80.

Ushindi huo umeifanya Singida Black Stars kuendelea kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo huku JKT Tanzania wakibaki nafasi ya sita.

Matokeo ya jana yameongeza ushindani katika mbio za nafasi za juu pamoja na vita ya timu zinazopambana kubaki Ligi Kuu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *