LIBASSE,MANQOBA WANG’ARA TUZO ZA LIGI KUU YA NBC AGOSTI.

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba ya Dar es Salaam, Libasse Gueye, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2026/27, huku Manqoba Mngqithi wa Young Africans, akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.

Gueye alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Maxi Nzengeli wa Young Africans na Oscar Mwajanga wa Mbeya City, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo mitano ambayo Simba ilicheza mwezi huo na kushinda yote, huku nyota huyo akifunga bao moja na kuhusika na mengine matano.

Kwa upande wa Manqoba aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Florent Ibenge wa Azam, aliiongoza Young Africans kushinda michezo yote mitano iliyocheza mwezi huo na kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Bukombe uliopo mkoani Geita,Deogratius Dayan kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Agosti kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

Kamati pia imeteua mabao matatu ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata bao bora la mwezi Agosti. Mabao hayo ni yaliyofungwa na Shekhan Hamis (Singida BS Vs Polisi Tanzania), Robert Mathias (Geita Gold Vs Kagera Sugar) na Hija Shamte (Mbeya City v Mashujaa)

Imetolewa na;

Idara ya Habari na Mawasiliano

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)

Septemba 11, 2026

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *