LIGI Kuu msimu wa 2026/27 imeendelea vyema ikiwa ni raundi ya sita kwa kuzikutanisha TRA United na Pamba Jiji, huku Pamba Jiji ikishindwa kufurukuta ikiwa uwanja wa nyumbani CCM Kirumba.
Mchezo huo ulishuhudia TRA United ikianza kwa kasi na kupata bao la kwanza dakika ya nne kupitia kwa mchezaji Ani Elijah kabla ya Nonyem Okorocha kuongeza bao la pili dakika ya saba baada ya kujifunga mwenyewe.
Jahazi la Pamba Jiji liliendelea kuzama baada ya mchezaji wa zamani wa Yanga Emmanuel Mwanengo kuongeza bao la tatu lililowapeleka TRA mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0.
Pamba jiji ilijaribu kurejea mchezoni na kupata bao dakika ya 76 kupitia kwa Abdulkarim Iddy ambalo halikuweza kuiepusha timu hiyo na kipigo na kujikuta ikipoteza kwa 3-1.Emmanuel Mwanengo,
Kwa upande mwingine katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera timu ya Kagera Sugar na Fountain Gate zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo ulioanza saa 1:00 usiku.
Kagera ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 26 kupitia Massanja Jesto kabla ya Fountain kusawazisha dakika ya 33 baada ya Andrew Vicent kujifunga mwenyewe.
Timu za Pamba Jiji na Kagera Sugar zinaendelea kuwa na rekodi mbaya msimu huu kwani hadi sasa hazijashinda mchezo wowote huku zikishika nafasi mbili za mwisho.