KIUNGO mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Berno Ngassa amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/27, huku Fikiri Elias wa Coastal Union akichaguliwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Ngassa alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo akiwashinda Maabad Maabad wa Coastal Union na Anuary Jabir wa Polisi Tanzania, alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa timu yake katika michezo miwili ambayo ilicheza mwezi huo na kushinda yote, huku nyota huyo akifunga bao moja na kuhusika na lingine moja.
Kwa upande wa Fikiri aliyeingia fainali na Steve Barker wa Simba na Vicent Mashami wa Dodoma Jiji, aliiongoza Coastal Union kushinda michezo yote miwili iliyocheza mwezi huo na kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi ya 11 kwenye msimamo wa ligi.
Kamati pia imeteua mabao matatu bora, ambayo yatapigiwa kura na mashabiki ili kupata bao bora la mwezi Septemba. Mabao hayo ni Haroun Lyawatwa (Mashujaa v Singida BS), Anuary Jabir (Polisi V Mbeya City) na Mohamed Damaro (Singida BS v Namungo).
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Ramadhan Kalanje wa KMC kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Septemba wa Ligi ya Championship ya NBC, akiwashinda Abiud Mtambuku wa Mbeya Kwanza na kipa Haroun Mandanda wa Rhino Rangers.
Kwa upande wa Kocha Bora wa ligi hiyo, kamati ilimchagua Mohamed Muya wa KMC aliyeiongoza timu yake kushinda michezo yote mitatu iliyocheza mwezi huo akiwashinda Salvatory Edward wa Rhino Rangers na Said Lyakuka wa Transit Camp alioingia nao fainali.