Baada ya mapumziko Ligi Kuu ya NBC inarejea tena leo kwa michezo mitatu ya mzunguko wa Saba, huku timu zikianza tena safari ya kusaka alama muhimu kuelekea mbio za ubingwa msimu huu.
Michezo hiyo itapigwa katika viwanja vitatu tofauti,kuanzia mchana hadi jioni, huku moja ya mechi zinazotarajiwa kuvutia hisia ikiwa ni pamba Jiji dhidi ya Geita Gold inayobeba taswira ya dabi ya Kanda ya Ziwa.
Mchezo wa kwanza utachezwa saa 8:00 mchana katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo Mashujaa itakuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania.
Macho ya mashabiki wengi wa soka yataelekezwa pia uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kuanzia saa 10:15 alasiri timu ya Pamba Jiji itakapokutana na Geita Gold.
Mchezo huo unaingia katika orodha ya mechi zenye mvuto mkubwa kwa kuwa ni dabi ya Kanda ya ziwa hivyo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Pamba jiji itatumia faida kucheza nyumbani na mbele ya mashabiki wake, wakati Geita Gold nayo itaingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kuondoka na alama muhimu.
Huko Lindi Namungo itakuwa mwenyeji wa TRA United katika mchezo utakaochezwa kuanzia saa 12:30 jioni kwenye uwanja wa Majaliwa.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa sehemu nyingine ya ushindani mkali wa raundi ya saba, huku timu zote zikilenga kuanza vyema baada ya mapumziko ya Ligi.