MASHUJAA, PAMBA JIJI NA NAMUNGO ZAREJEA KIBABE LIGI KUU YA NBC.

TIMU za Mashujaaa, Pamba Jiji na Namungo zimeanza kwa ushindi baada ya mapumziko ya Ligi Kuu ya NBC ya msimu wa 2026/27 kufuatia matokeo ya michezo mitatu ya mzunguko wa saba.

Mchezo wa Kwanza ulipigwa kwenye uwanja wa Lake Tanganyika uliowakutanisha Wenyeji Mashujaa na Polisi Tanzania na Mashujaa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Mashujaa iliyoanza kupata bao kupitia kwa Mishamo Michael dakika ya 30 akiipa timu yake matumaini ya kubaki na alama tatu nyumbani.

Hata hivyo Polisi ilirejea mchezoni katika kipindi cha pili kupitia kwa Anuary Jabir akifunga bao la kusawazisha dakika ya 52 kwa mkwaju wa penati na kurejesha ushindani katika mchezo huo.

Mchezo ulionekana kuelekea kumalizika kwa sare lakini Michael Godlove aliibuka shujaa wa Mashujaa kufunga bao la ushindi kwa Penati dakika ya 90+5 na kuifanya timu hiyo kuondoka na alama zote tatu mbele ya mashabiki wake.

Katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Pamba Jiji ilikutana na Geita Gold katika pambano lililokuwa na mvuto wa kipekee kwa mashabiki wa Kanda ya ziwa ambapo Pamba iliibuka na ushindi wa 4-0 ikiwa ushindi wa kwanza msimu huu.

Pamba jiji ilianza kwa kasi na kupata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia Henry Msabila kabla ya Deogratias Mafie kuongeza la pili dakika ya 18 na kuifanya timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa na faida ya mabao mawili.

Kipindi cha pili kilirejea kwa Pamba Jiji kuendelea kutawala mchezo, alikuwa Zabona Mayombya akifunga bao la tatu dakika ya 50 na kuimarisha zaidi nafasi ya wenyeji.

Diomande Idris alihitimisha ushindi huo mnono kwa kufunga bao la nne dakika ya 79 na kuifanya Pamba Jiji kuondoka na ushindi wa mabao 4 -0 mbele ya mashabiki wake wa Mwanza.

Huko mkoani Lindi, Namungo imetumia vyema faida ya kucheza nyumbani baada ya kuichapa TRA bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa Ruangwa majira ya saa 12:30 jioni.

Bao la pekee la mchezo huu lilifungwa na Helbert Lukindo dakika ya 11 akiwezesha Namungo kupata uongozi wa mapema na kuanza safari ya kusaka ushindi.

Baada ya bao hilo timu zote ziliendelea kupambana kusaka matokea lakini Namungo ilifanikiwa kulinda uongozi wake hadi dakika 90 zilizokamilika na hivyo kujikusanyia alama tatu muhimu.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *