Timu ya Simba imeibuka na ushindi kwenye dabi ya Kariakoo baada ya kuifunga timu ya Young Africans bao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliochezwa Oktoba 10 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar-es Salaam.
Mchezo huo ulioanza majira ya saa 1:00 usiku ulikuwa muhimu kwa timu zote ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC baada ya timu hizo kucheza takribani michezo sita bila kupoteza.
Mchezo ulianza kwa kasi na timu zote kushambuliana na iliwachukua dakika tano timu ya Young Africans kufungua ukurasa wa mabao kupitia mshambuliaji wake Peter Shalulile aliyepokea pasi kutoka kwa Maxi Nzengeli bao lililodumu hadi mwisho wa kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilirejea huku Simba wakishambulia kwa kasi ambapo Kocha Steve Barker aliamua kufanya mabadiliko kwa kumtoa Chama na kumuingiza Keletso Makgalwa na dakika ya 67 kiungo wa Simba Neo Maema aliifungia timu yake bao la kwanza hivyo ubao kusomeka 1-1.
Dakika ya 71 Ellie Mpanzu aliiandikia timu ya Simba bao la pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Keletso Makgalwa hivyo ubao kusomeka 2-1.
Dakika 90 zilitamatika katika dimba la Uhuru kwa Simba kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya mtani wake na mpinzani wake wa karibu katika Ligi Kuu ya NBC na mchezaji wa Simba Ellie Mpanzu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.