LIGI Kuu ya NBC inaendelea kushuhudia ushindani huku macho ya mashabiki wa soka yakielekezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mkoani Dar es Salaam, ambako timu ya JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mbeya City katika mchezo unaotarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku.
Mchezo huo unawakutanisha wapinzani wanaotofautiana kwa nafasi moja tu kwenye msimamo wa ligi, ambapo Mbeya City inashika nafasi ya nane huku JKT Tanzania ikiwa nafasi ya tisa.
Hali hiyo inaufanya mchezo huu kuwa mgumu na muhimu kwa timu zote mbili katika harakati za kuboresha nafasi zao walizopo kwenye msimamo.
JKT kucheza uwanja wa nyumbani ni nafasi ya kutumia faida ya uwanja wao kujipatia alama muhimu mbele ya mashabiki wao.
Wanajeshi hao wanahitaji kuonyesha nidhamu, umakini na uwezo wa kutumia nafasi wanazozitengeneza ili kupata matokeo yatakayowapa nafasi ya kuisogelea Mbeya City kwenye msimamo.
Kwa upande wa Mbeya City, safari ya kwenda Isamuhyo ina changamoto yake, lakini pia ni fursa ya kuthibitisha ushindani wao dhidi ya timu wanayoizidi kwa nafasi moja pekee kwenye msimamo.
Matokeo chanya yatawapa nafasi ya kuimarisha nafasi yao na kwenda pazuri zaidi na kuendeleza ushindani katika Ligi Kuu ya NBC na alama tatu thamani yake ni zaidi ya ushindi.
Kwa timu ya JKT Tanzania ushindi unaweza kuwa hatua muhimu ya kuipiku Mbeya City, huku wageni hao wakitafuta matokeo yatakayowasaidia kupanda nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa ligi.
Hata hivyo nafasi za timu kwenye msimamo pekee haziamui matokeo ya mchezo, Nidhamu ya kiufundi, umakini katika safu ya ulinzi na ufanisi wa washambuliaji wa timu hizo vinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatma ya dakika 90 itakavyokuwa.