JABIR ANAKITAKA KIATU CHA UFUNGAJI BORA LIGI KUU YA NBC.

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Anuary Jabir, ameendelea kung’ara katika mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027, akiongoza orodha ya wafungaji kwa mabao saba, akiwazidi washindani wake wanaofuatia kwa tofauti ya mabao matatu.

Jabir anaongoza katika orodha hiyo akiwa amecheza michezo tisa sawa na dakika 742 ndani ya msimu wa 2026/2027 wa Ligi Kuu ya NBC.

Wachezaji sita wa timu mbalimbali wamefuatia kwenye orodha hiyo kwa kufungana kwa mabao manne kila mmoja, hali inayofanya ushindani wa kuwania nafasi za juu katika orodha ya wafungaji kuwa mkubwa baada ya mizunguko tisa ya Ligi hiyo.

Peter Shalulile wa Young Africans hayuko mbali akifanikiwa kufunga mabao manne ndani ya dakika 507 za Ligi Kuu ya NBC saw ana michezo saba.

Elie Mpanzu na Clatous Chama wa Simba kila mmoja anayo mabao manne Mpanzu akitumia michezo nane sawa na dakika 528 huku Chama akitumia dakika 567 kwenye michezo saba kuhakikisha anapata mabao manne.

Herbert Lukindo wa timu ya Namungo ndio anafuata akicheza michezo sita sawa na dakika 336 amefanikiwa kufunga mabao manne pia ndani ya msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC.

Obrey Chirwa wa timu ya Geita Gold amecheza dakika 536 sawa na michezo saba akiingia nyavuni mara nne na kuisaidia timu yake kupata alama.

Abdul Suleiman wa timu ya Azam naye kaweka nyavuni mabao manne mpaka sasa akicheza dakika 297 ndani ya michezo mitano ya Ligi Kuu ya NBC.

Safari bado ni ndefu huku kila mchezo ukiwa na nafasi ya kubadilisha mwelekeo wa ushindani huo. Swali kubwa linabaki kuwa je, Anuary Jabir ataendelea kutawala orodha hiyo au washindani wake wataongeza kasi na kumkaribia? Jibu tutalipata kadri utamu wa Ligi Kuu ya NBC unavyozidi kunoga.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *