Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema ubora wa Ligi Kuu ya NBC umeendelea kuimarika kutokana na matumizi ya teknolojia mbalimbali, ikiwemo mfumo wa Football Video Support (FVS), ambao umesaidia kupunguza malalamiko yanayohusu maamuzi ya waamuzi.
Karia ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa 13 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania uliofanyika katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia yamekuwa nyenzo muhimu katika kuboresha usimamizi na uendeshaji wa ligi pamoja na kuongeza usahihi wa maamuzi ndani ya uwanja.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia mfumo wa FVS katika mashindano ya ligi, huku jumla ya mechi 240 zikiwa zimejumuishwa katika mfumo huo. Aidha, ameeleza kuwa mechi 150 zinapaswa kuwasilishwa na kuripotiwa kupitia mfumo huo ili kuhakikisha matumizi yake yanaendelea kuwa na tija.
Kwa mujibu wa Karia, matumizi ya teknolojia hiyo yamechangia kupunguza malalamiko yanayohusu maamuzi ya waamuzi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuinua viwango vya soka nchini na kuongeza imani ya wadau katika usimamizi wa mashindano.
Katika hatua nyingine, mkutano huo ulimchagua Ndugu Joan Mazanda kuwa mjumbe mwakilishi wa klabu za Ligi Kuu katika kamati tendaji ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, baada ya kupata ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu.
Matumizi ya teknolojia katika soka yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya mchezo huo, yakilenga kuongeza uwazi, haki na ubora wa mashindano kwa manufaa ya klabu, wachezaji, waamuzi na wadau wote wa soka nchini.