LIGI ya Championship ya NBC msimu wa 2026/2027 inaendelea huku ushindani mkali ukiendelea baada ya timu zote kucheza mizunguko 10, huku Mtibwa Sugar ikishika usukani wa ligi hiyo kwa kukusanya pointi 21.
Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imejikusanyia alama hizo baada ya kushinda michezo sita, kutoka sare tatu na kupoteza mchezo mmoja, ikiwa imefunga mabao 13 na kuruhusu saba, hivyo kuwa na tofauti ya mabao sita.
Katika nafasi ya pili ipo Tanzania Prisons kutoka Mbeya yenye alama 20, ikiwa imecheza michezo 10, ikishinda sita, kutoka sare mbili na kupoteza miwili. Prisons imeonyesha makali zaidi katika safu ya ushambuliaji kwa kufunga mabao 15 na kuruhusu sita.
KMC ya Dar es Salaam inashika nafasi ya tatu kwa pointi 19, ikiwa na ushindi mara tano, sare nne na kipigo kimoja. Timu hiyo imekuwa na rekodi nzuri ya ufungaji baada ya kufikisha mabao 17, huku ikiruhusu saba pekee.
Bandari Tanzania inakamilisha nne bora ikiwa na pointi 18, ikifuatiwa na Transit Camp na Rhino Rangers ambazo kila moja ina pointi 16, zikishika nafasi ya tano na sita.
Katika sehemu ya katikati ya msimamo, ushindani nao ni mkubwa, huku Gunners ipo nafasi ya saba, Stand United ipo nafasi ya nane na Mbuni iliyopo nafasi ya tisa zikiwa zimekusanya alama 14 kila moja, zikifuatiwa na Bigman nafasi ya 10 yenye alama 13.
Kwa upande wa chini ya msimamo, Kigamboni United nafasi ya 11 na KenGold iliyopo nafasi ya 12 zina alama 12 kila moja, IAA iliyopo nafasi ya 13 ina alama 11, huku Tabora United iliyo nafasi ya 14 ikiwa na alama saba.
Kwa upande wa nafasi ya 15 ipo Songea United yenye pointi sita na nafasi ya 16 ni timu ya TMA yenye alama mbili ndizo zinazoshika nafasi mbili za mwisho baada ya michezo 10.
Safari ya NBC Championship ikiendelea, kila mchezo unazidi kuwa muhimu kwa timu zinazowania nafasi za kupanda Ligi Kuu, huku zile za chini zikihitaji kupambana zaidi kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.