Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inapenda kuufahamisha umma, wadau na
mashabiki wa soka kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeingia makubaliano na
mdau mpya wa huduma za tiketi, lipa financial solutions (lipa tickets), ambaye
atasimamia mfumo wa uuzaji na usimamizi wa tiketi katika michezo ya Ligi Kuu ya
NBC.
Kupitia mfumo huu, mashabiki wataweza kununua tiketi zao kwa njia rahisi na
salama kupitia simu zao za mkononi bila kulazimika kufika kwenye vituo vya
mauzo ya tiketi.
Ununuzi wa tiketi utafanyika kupitia njia zifuatazo:
1. Tovuti ya Tiketi: Tembelea www.tickets.ligikuu.tz na kufuata maelekezo ya
ununuzi wa tiketi.
2. Tovuti ya TPLB: Tembelea tovuti rasmi ya Bodi ya Ligi, www.ligikuu.co.tz,
kisha bofya kiunganishi cha ununuzi wa tiketi (Match Tickets).
3. USSD: Piga *149*46*11# kupitia simu yako na ufuate maelekezo
yatakayotolewa ili kukamilisha ununuzi wa tiketi.
Utaratibu wa kuingia uwanjani baada ya kununua tiketi
Baada ya kukamilisha malipo ya tiketi, utaratibu wa kupokea uthibitisho wa
ununuzi na kuingia uwanjani utakuwa kama ifuatavyo:
Watumiaji wa simu za kawaida (Feature Phones): Baada ya kukamilisha
ununuzi, mnunuzi atapokea msimbo maalumu (Code) kupitia ujumbe mfupi
wa simu (SMS), ambao atauonyesha getini ili kuhakikiwa na kuruhusiwa
kuingia uwanjani.
Watumiaji wa simu janja (Smartphones): Baada ya kukamilisha malipo,
mnunuzi atapokea tiketi yenye alama maalumu ya QR Code, ambayo
ataitumia wakati wa kuhakikiwa kwenye lango la kuingilia uwanjani.Mfumo huu umeandaliwa kwa namna inayomwezesha kila shabiki kununua tiketi
kwa urahisi, iwe anatumia simu janja au simu ya kawaida, hivyo kutoa fursa sawa
kwa mashabiki wote kupata huduma hiyo.
TPLB inaendelea kuboresha mifumo ya uendeshaji wa ligi kwa kutumia teknolojia
ili kurahisisha huduma kwa mashabiki, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa tiketi
na kuboresha uzoefu wa mashabiki wanapohudhuria michezo ya Ligi Kuu ya NBC.
Imetolewa na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).