LIGI Kuu ya NBC inarejea kwa tena kesho Novemba 20, baada ya mapumziko yaliyotokana na michezo ya kufuzu AFCON pamoja na michezo ya kalenda ya FIFA ligi hiyo itaendelea kwa raundi ya 12 ikianza kwa michezo mitatu.
Mapumziko hayo yamezipa timu nafasi ya kufanya tathmini ya mwenendo wao kurekebisha mapungufu na kujiandaa kwa hatua inayofuata ya msimu huku baadhi ya wachezaji wakipata nafasi ya kuiwakilisha nchi zao katika majukumu ya kimataifa.
Raundi ya 12 itaanza kwa mchezo kati ya Polisi Tanzania wakiwakaribisha Young Africans kwenye uwanja wa ushirika, Kilimanjaro saa 10:00 alasiri. Yanga wanaingia katika mchezo huo wakitamani kuendeleza ushindani wao huku Polisi Tanzania wao wakitamani kutumia uwanja wao wa nyumbani kupata matokeo mbele ya mabingwa hao watetezi.
Mchezo mwingine utakuwa kati ya Namungo dhidi ya Mbeya City utakaopigwa katika uwanja wa Majaliwa saa 12:30 jioni. Namungo watakuwa na jukumu la kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani huku Mbeya City wakisaka matokeo mazuri ugenini.
Mchezo mwingine wa kuvutia utakuwa kati Azam na Singida Black Stars utakaopigwa katika uwanja wa Azam complex saa 3:00 usiku na watakutana wakiwa na kiu ya kuendeleza ushindani wa ligi, huku mchezo huo ukiwa na mvuto kutokana na ubora wa vikosi vya pande zote mbili na timu zote zikiiwakilisha Tanzania kimataifa.
Kipekee Azam, Singida Black Stars na Yanga zinaingia katika ratiba zikiwa zimetoka kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu ya CAF, hali itakayoongeza mvuto wa michezo yao kutokana na uzoefu wa ushindani wa kimataifa walioupata.