LIGI KUU YA NBC IMEFIKIA PATAMU.

LIGI Kuu ya NBC imeendelea jana baada ya mapumziko ya kalenda ya Fifa ambapo mzunguko wa 12 wa Ligi hiyo umeanza rasmi jana kwa michezo mitatu iliyochezwa viwanja mbali mbali nchini.

Mchezo wa kwanza ulikuwa katika uwanja wa Ushirika mkoani Kilimanjaro ambapo Polisi Tanzania ilikuwa mwenyeji wa timu ya Young Africans katika mchezo ulichezwa saa 10:00 alasiri.

Iliwachukua dakika 29 timu ya Young Africans kufungua ukurasa wa mabao kupitia mshambuliaji wake Cheikh Toure na ubao ulisoma 0-1 hadi muda wa mapumziko.

Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi Polisi wakijaribu kusawazisha lakini dakika ya 75 mshambuliaji wa Young Africans, Peter Shalulile aliiongezea timu yake bao la pili hivyo mchezo kutamatika kwa matokeo ya 0-2 na kiungo wa timu ya Young Africans Aziz Ki alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Mchezo wa pili ulichezwa katika uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi ambapo Namungo ilikuwa mwenyeji wa timu ya Mbeya City katika mchezo uliochezwa majira ya saa 12:00 jioni.

Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikitaka alama tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ambapo hadi dakika 45 zinatamatika sio mwenyeji wala mgeni ambaye aliweza kupenya kwenye nyavu za mwenzake.

Kipindi cha pili kilirudi kwa kasi kila timu ikitaka kuonyesha ubabe wake kwa mwenzake hata hivyo mbinu hazikufua dafu kwani mchezo ulitamatika kwa matokeo ya suluhu na golikipa wa Mbeya City Brighton Munthali alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo kwa kiwango kizuri alichokionyesha.

Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya NBC jana ulichezwa majira ya saa tatu usiku katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Dar es Salaam ambapo Azam ilikuwa mwenyeji wa timu ya Singida Black Stars.

Azam ilianza mapema kulisaka lango la mpinzani wao ambapo dakika 27 zilimtosha kiungo wa timu hiyo Feisal Salum kufungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati na dakika ya 29 Zidane Sereri aliiongezea bao timu hiyo kwa pasi ya Iddi Seleman hivyo ubao kusoma 2-0.

Dakika ya 40 Singida ilipata bao la kwanza kupitia mchezaji wake Emmanuel Keyekeh ambapo mpaka dakika 45 zinatimia ubao ulisoma 2-1.

Kipindi cha pili kilirejea ambapo kila timu ilikuwa ikipambana kupata alama tatu hata hivyo dakika ya 60 mchezaji wa Singida James Mwashinga aliisawazishia bao timu yake na dakika ya 68 na 72 mshambuliaji wa timu hiyo Jonathan Sowah aliongeza mabao mawili hivyo matokeo kuwa 2-4 hadi mchezo unatamatika.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars Jonathan Sowah alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

Ligi Kuu ya NBC itaendelea leo kwa michezo mitatu ya Pamba Jiji dhidi ya Coastal Union katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza, JKT Tanzania itaiakaribisha Simba katika uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Dar es Salaam na Dodoma Jiji itakuwa mwenyeji wa Fountain Gate katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Start a Conversation

Your email address will not be published. Required fields are marked *