Michezo mitatu ya Ligi Kuu ya NBC imeendelea na kushuhudia ushindi kwa Pamba Jiji na Simba, huku Fountain Gate na Dodoma jiji zikitoshana nguvu baada ya kutoka suluhu.
Mchezo wa kwanza ulianza majira ya saa 10:00 jioni uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza ambapo Pamba jiji walipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliokuwa na msisimko na ushindani hadi dakika ya mwisho.
Abdoulaye Camara alianza kuifungia Pamba Jiji dakika ya tisa, kabla ya Maabad Maabad kuifungia Coastal Union bao dakika ya 14, pamba Jiji iliongeza lingine dakika ya 38 na Maabad Maabad alisawazishia tena Coastal dakika ya 54 hivyo kuweka mzani sawa.
Dakika ya 90+5 Abdulrahim Bausi aliwanyanyua mashabiki wa Pamba Jiji na kuipa timu yake alama tatu muhimu.
Katika mchezo mwingine uliochezwa uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo,Dar es saalam majira ya 12:30 Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2 -1 dhidi ya JKT Tanzania.
JKT Tanzania ndiyo iliokuwa ya kwanza kupata bao la dakika ya 10 kupitia kwa Said Mkopi ambae aliwapa furaha ‘maafande’ katika uwanja wao wa nyumbani.
Simba ilirejea mchezoni kwa kusawazisha kupitia kwa Elie Mpanzu dakika ya 20, Libasse Gueye alihakikisha anawapa furaha mashabiki kwa kufunga bao la pili dakika ya 34 na kuifanya timu hiyo kuwa na ushindi wa 11 kwenye michezo 11.
Mchezo wa mwisho ulichezwa uwanja wa Jamhuri, Mkoani Dodoma majira ya saa 3:00 usiku kati ya wenyeji Dodoma Jiji na Fountain Gate ulimalizika kwa suluhu na kufanya kila timu kujikusanyia alama moja.
Kwa ujumla michezo hiyo mitatu imezalisha jumla ya mabao nane huku Simba ikiendelea kushikilia usukani wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kukusanya alama 33 hadi sasa.