MZUNGUKO wa 11 wa Ligi ya Championship ya NBC umetamatika baada ya michezo yote nane kuchezwa kwenye viwanja mbali mbali nchini.
Novemba 20 ilichezwa michezo mitatu majira ya saa kumi jioni ambapo Bigman iliikaribisha timu ya Bandari Tanzania katika uwanja wa Mkwakwani Tanga na mchezo ulitamatika kwa Bigman kushinda 1-0.
Mchezo wa pili ulichezwa uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo Kigamboni United ilikuwa mwenyeji wa Rhino Rangers na mchezo ulitamatika kwa Kigamboni kuibuka na ushindi wa 2-1.
Stand United iliialika timu ya Transit Camp uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga na mchezo uliweza kutamatika kwa suluhu.
Novemba 21 michezo mitatu ya mzunguko wa 11 ilichezwa pia ambapo Mtibwa Sugar ilikuwa mwenyeji wa timu ya Gunners katika uwanja wa Manungu mkoani Morogoro ambapo mchezo ulitamatika kwa Mtibwa kuibuka na ushindi wa 2-1.
TMA ilicheza na timu ya KMC katika uwanja wa Samora mkoani Iringa majira ya saa kumi jioni na mchezo ulitamatika kwa sare ya 1-1.
Kengold ilikutana na timu ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Manispaa ya Chunya na mchezo ulitamatika kwa mwenyeji kukubali kichapo cha 1-2.
Novemba 22 michezo miwili imechezwa kutamatisha mzunguko wa 11 wa Ligi ya Championship ya NBC ambapo Tabora United imecheza na Songea United uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mkoani Tabora na mchezo umetamatika kwa Tabora kushinda 3-1.
Mchezo wa mwisho kwa mzunguko wa 11 wa Ligi ya Championship ya NBC ulikuwa jijini Arusha ambapo timu ya Mbuni ilikuwa mwenyeji wa timu IAA katika uwanja wa Aga Khan na mchezo uliisha kwa sare ya 1-1.