Timu ya Geita Gold imeendeleza ushindani wake kwenye Ligi Kuu NBC msimu wa 2026/27 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa raundi ya 13 uliochezwa uwanja wa Bukombe mkoani Geita.
Geita ilianza kuonyesha makali yake dakika ya 40 kupitia kwa mshambuliaji Obrey Chirwa alieipatia bao la kwanza na kuipa nafasi ya kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilikuwa na kasi zaidi ambapo Geita Gold iliendelea kuutawala mchezo na kupata bao la pili dakika ya 57 kupitia Martin Kigi,kabla ya Maulid Shabani kuongeza bao la tatu dakika ya 62.
Dakika moja baadaye Coastal Union ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa mchezaji wake Maabad Maulid aliyefanikiwa kupenya ukuta wa Geita Gold na kupunguza pengo la mabao huku akifunga bao lake la sita msimu huu.
Hata hivyo matumaini ya Coastal union kurejea mchezoni yalizimwa dakika ya 87 baada ya Yusuph Mhilu kufunga bao la nne kwa Geita Gold kupitia mkwaju wa Penalti na kuhitimisha ushindi wa mabao 4-1.
Na mchezaji bora wa mchezo huo alikuwa Martin Kigi wa Geita Gold.