Timu ya Pamba Jiji na Namungo zimegawana alama baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 huku Kagera Sugar na Dodoma Jiji zikishindwa kufungana katika michezo miwili ya Ligi Kuu ya NBC.
Katika mchezo wa wa kwanza uliochezwa majira ya saa 10:00 alasiri kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, Pamba Jiji waliwakaribisha Namungo na kupeana zamu ya kupata mabao kabla ya kumaliza dakika 90 kwa 2-2.
Namungo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 51 kupitia kwa Nassoro Kapama aliyefunga kwa mkwaju wa Penalti ambalo hata hivyo dakika ya 60 Pamba Jiji ilisawazisha kupitia bao la kujifunga la Rogers Gabriel.
Pamba jiji ilipata bao la pili dakika ya 77 baada ya Abdallah Ali wa Namungo kujifunga lakini Namungo ilirejea mchezoni dakika ya 87 kupitia Natanael Iga aliyefunga bao la kusawazisha na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 2-2.
Katika mchezo mwingine uliopigwa majira ya saa 1:00 usiku kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera wenyeji Kagera Sugar walilazimika kuridhika na sare ya kutokufungana dhidi ya wageni wao Dodoma Jiji.
Walipambana kupata mabao katika kipindi chote cha mchezo lakini safu zao za ushambuliaji zilishindwa kutumia nafasi walizopata na kuishia kugawana alama baada ya dakika 90 bila timu yeyote kutikisa nyavu.
Ushindani wa ligi Kuu ya NBC utaendelea leo ambapo Mashujaa inatarajia kuwa mwenyeji wa walipa kodi TRA United katika mchezo utakaochezwa majira ya saa 10:00 jioni kwenye uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.